Habari za Kitaifa

Polisi waruka PCEA kuhusu wahuni waliovamia Gachagua 

Na KEVIN CHERUIYOT April 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SIKU moja baada milio ya risasi, majeruhi na tendabelua kushuhudiwa katika Kanisa la Kipresbaiteri cha Afrika Mashariki (PCEA) Mwiki, Kasarani, Nairobi, uongozi wa kanisa hilo umetoa maelezo kuhusu kisa hicho.

Mnamo Jumapili, Aprili 6, 2025, shughuli ya kuchangisha pesa za kukamilisha mradi wa ujenzi wa kanisa la PCEA ilikumbwa na fujo wahalifu walipolivamia dakika chache baada ya aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua kuwasili.

Polisi wenye sare rasmi hawakuonekana wakati wa milio ya risasi huku walinzi wa kibinafsi walioandamana na Bw Gachagua wakikabiliana na wahalifu hao, waliosikika wakiitisha pesa.

Hata hivyo, kulingana na mmoja wa viongozi wa kanisa hilo waliozungumza na Taifa Leo, kituo cha polisi cha Mwiki kilichoko umbali wa kilomita moja kutoka hapo, kilikuwa na habari kwamba kungekuwa na shughuli kubwa.

Kiongozi huyo wa PCEA, Mwiki, ambaye aliomba tubane jina lake, alikiri kuwa hawakuarifu kituo hicho kwa njia rasmi.

“Tulijulisha polisi siku moja kabla, japo kwa njia ya mdomo kwani hatukuwa na uhakika kuwa wanasiasa wangehudhuria,” akaeleza.

Kanisa hilo lilisema halikuwa na uhakika kwamba Bw Gachagua angehudhuria shughuli ya kuchangisha pesa licha ya kwamba awali aliwadokezea kuwa angeshiriki mchango kanisani humo.

“Hata hivyo, hatukuwa na uhakika kabisa kwamba angefika…………. Hiyo ndio maana hatukuwaandikia polisi barua rasmi kuomba ulinzi,” kiongozi huyo wa PCEA akaeleza.

Hata hivyo, kupitia taarifa Jumatatu jioni, Aprili 7, 2025, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ilisema kuwa polisi hawakujulishwa kuhusu shughuli hiyo.

“Isitoshe, afisa msimamizi wa kituo cha polisi cha Mwiki amesema kuwa kanisa hilo lilifeli kujulisha afisi yake kwamba shughuli hiyo ingehudhuriwa na wanasiasa na hivyo wangehitaji maafisa wa polisi watumwe hapo mapema,” DCI ikasema.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Mwiki waliosikia milio ya risasi katika kanisa hilo walielekea huko kuwakabiliwa wahalifu hao waliotoroka na utulivu ukarejelea.

“Wengi wao walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Mwiki. Pikipiki 10 pia zilinaswa na kuzuiwa katika kituo hicho cha polisi,” DCI ikasema.