Habari za Kitaifa

Hofu kuondolewa kwa ufadhili kunahatarisha afya ya kina mama wajawazito

Na LUCY KILALO April 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KUONDOLEWA kwa ufadhili muhimu Barani Afrika uliodhaminiwa na Amerika, hasa ule wa USAID, kunahatarisha afya ya kina mama wajawazito.

Hivi leo, kuna uwezekano mkubwa zaidi kuliko hapo awali wa wanawake kunusurika wakati wa ujauzito na kujifungua – ripoti yaonyesha.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN), Trends in maternal mortality imeonyesha kuwa kumekuwa na upungufu wa asilimia 40 wa vifo vya akina mama duniani kati ya mwaka 2000 na 2023.

Upungufu huu umechangiwa na kuongezeka kwa huduma muhimu za afya.

Hata hivyo, ripoti hii imetolewa wakati ufadhili wa misaada ya kibinadamu unapunguzwa kwa kiasi kikubwa na mashirika ya UN yanaonya kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, wanawake wajawazito wataumia.

Hii ni kwa sababu ufadhili huu ulikuwa unasaidia matibabu ya malaria, kudhibiti shinikizo la damu (pre-eclampsia) na mama kutokwa na damu sana wakati anajifungua (haemorrhage).

Mwaka wa 2021, wanawake wapatao 40,000 walifariki kutokana na matatizo ya ujauzito.

Idadi hiyo iliongezeka hadi 322,000 kutoka 282,000 mwaka uliopita.