Makala

Kang’ata aanza kuzawidi wanaooa kisheria na kuzaa

Na MWANGI MUIRURI April 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kaunti ya Murang’a inakusudia kutenga Sh200 milioni katika mwaka wa fedha wa 2025/26 kugharamia huduma za afya kwa makundi ya watu walio katika hatari.

Mbali na kugharamia gharama za matibabu, mpango huu utawazawidi wanachama Sh10,000 wanapooa kisheria, na Sh10,000 wakizaa mtoto wao wa kwanza.

Hii itafanya jumla ya uwekezaji katika mpango wa Kang’ata Care kufikia Sh400 milioni tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, ambapo wakati huo ulikuwa na bajeti ya Sh200 milioni.

Licha ya kuongezeka kila mwaka kwa idadi ya wanaonufaika, bajeti imekuwa ile ile

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Afya katika kaunti ya Murang’a Eliud Maina, bajeti hii inapendekezwa chini ya kipengele cha mpango wa Kang’ata Care, unaolenga kuboresha maisha ya watu maskini.

“Hadi sasa, tumesajili familia 40,000 zinazowakilisha takriban watu 160,000. Mradi huu unatoa zawadi ya Sh10,000 kwa wanachama wanaooa kisheria, na pia zawadi ya Sh10,000 wakizaa mtoto wao wa kwanza,” alisema Bw Maina.

Alitaja mpango huu kama motisha ya kijamii iliyoundwa kudumisha hadhi ya maisha ya watu walio katika hatari na kuwafanya wahisi kuthaminiwa, kusaidiwa, na kuheshimiwa.

“Tuna wanachama ambao bado hawajaolewa, lakini tunagharamia bima zao za afya nje ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Wanachama wetu ni wa kati ya umri wa miaka 25 na 75. Ili kujiunga na mpango huu, mtu lazima aoe rasmi na kuwasilisha cheti cha ndoa kilichothibitishwa,” alisema.

Bw Maina aliongeza, “Haijalishi kama ulikuwa katika ndoa ya njoo tuishi pamoja. Mara tu unapohalalisha ndoa hiyo kisheria, utapokea Sh10,000 zako.”

Alifafanua pia kuwa mtu anayenufaika akifariki na mke/mume wake aoe tena kisheria, katika ndoa mpya, wanandoa watakuwa na haki ya kupokea msaada wa Sh10,000.

“Wanaonufaika watapokea pesa hizi kwa kuwasilisha cheti cha ndoa na cheti cha kuzaliwa mtoto wao. Baadhi wameuliza kama tutahitaji vipimo vya DNA kuthibitisha uzazi. Kwa sasa, cheti cha kuzaliwa kinatosha,” aliongeza.

Mnamo Aprili 15, 2025, Serikali ya Kaunti ilitumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii kujitetea kuhusu mpango huu, ikisema kuwa haukusudiwi kuongeza idadi ya watu wa Murang’a, ambayo ilikuwa 1.05 milioni 1.05 katika sensa ya 2019.

“Manufaa haya yanapatikana tu kwa wanachama wa Kang’ata Care. Si kila mkazi wa Murang’a anamiliki kadi ya kusajiliwa. Huu ni mpango wa bima kwa familia za watu walio katika hatari, unaotoa manufaa matatu:  usaidizi wa gharama za mazishi wa Sh100,000, na zawadi kwa  kuoa na kuzaa mtoto ya Sh10,000,”  lilisema chapisho hilo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Bunge la Kaunti ya Murang’a, John Mwangi, alisema kuwa Bunge limethibitisha mpango huu na kuamua kuunga mkono kisheria na kimaadili.

Alisema kuwa bajeti ya mpango huo itaongezeka kila mwaka kadri wanachama wanavyosajiliwa.

Kiongozi wa Wengi wa Bunge la Kaunti ya Murang’a, Gichobe Mbatia, alitaja mpango huo kama  “ubunifu na mageuzi,” akisema kwamba vigezo vya kutambua wanaonufaika vimewekwa wazi.

Mnamo Aprili 14, 2025, Gavana Irungu Kang’ata alitumia akaunti yake rasmi ya X kuwakaribisha wanachama wa Kang’ata Care walioolewa hivi karibuni kudai zawadi zao.

“Je, uko katika Kang’ata Care na umeoa rasmi? Dai zawadi yako katika Hospitali ya Murang’a Level Five. Ni haki yako,” aliandika katika chapisho hilo.