Makala

Pesa za wanasiasa zinavyogawanya makanisa nchini

Na  CHARLES WASONGA April 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MGAWANYIKO mkubwa umeshuhudiwa katika makanisa nchini kuhusu michango ya fedha kutoka kwa wanasiasa, makanisa makubwa yakipinga huku madogo yakishabikia.

Nalo Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK) limepiga marafuku mwenendo wa wanasiasa kutangaza matoleo yao makanisani, likisema hatua hiyo inashusha hadhi ya maeneo hayo ya kuabudu.

Kwenye taarifa kwa wanahabari Machi 23, 2025 baada ya kuongoza mkutano wa baraza kuu mjini Limuru, Kaunti ya Kiambu, mwenyekiti Askofu Elias Agola alishauri viongozi wa makanisa kutokubali michango mikubwa ya fedha ambayo asili yao haijulikani kutoka kwa wanasiasa.Aidha, NCCK ilitoa miongozo minane ya kudhibiti siasa na matoleo madhabahuni.

“Matoleo yoyote ya wanasiasa yachukuliwe kama sadaka ya kawaida na hayafai kutangazwa hadharani,” alieleza akitaja moja ya miongozo hiyo.Agizo hilo lilijiri siku chache baada ya kiongozi wa Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK), Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit, kupiga marufuku wanasiasa kutoa mamilioni ya pesa makanisani na kutangazia waumini.

Aidha, Ole Sapit alizima wanasiasa kupewa nafasi kuhutubia waumini ndani ya makanisa akisema “inachafua utakatifu wa nyumba ya Mungu.”

“Kanisa sio mahala pa wanasiasa kuendeleza ajenda zao. Hatulengi wanasiasa walioko hapa, ila wanasiasa wote watakaohudhuria ibada za Jumapili katika makanisa yote ya ACK nchini,” akaeleza katika Kanisa la ACK St Peters Jogoo Road, Nairobi, mwezi jana.

Awali, Novemba iliyopita kiongozi wa Kanisa Katoliki Nchini, Askofu Mkuu Philip Anyolo, aliagiza uongozi wa kanisa la Soweto, Nairobi, kurejesha mchango wa Sh5.8 milioni kutoka kwa Rais William Ruto.

Kulingana na Anyolo, mchango huo ulitolewa kinyume na hitaji la Sura ya Sita ya Katiba na Sheria kuhusu Maadili na Uongozi Bora 2003.Hata hivyo, makanisa mengine, haswa yale madogo, yamechukua msimamo tofauti na kutangaza wazi kuwa yataendelea kupokea michango na matoleo ya wanasiasa.

Mapema mwaka huu Kanisa la Pentecostal Evangelistic Fellowship of Africa (PEFA) liliunga mkono michango ya wanasiasa makanisani likisema “sio sawa kurejesha kwa sababu zimetolewa na wanasiasa.”

Hii ni licha ya mienendo hiyo kuwakera Wakenya wanaopitia hali ngumu kiuchumi huku sekta muhimu kama afya na elimu zikibaliwa na changamoto za kifedha.

“Kama kanisa la PEFA hatuwezi kurejesha pesa ambazo wanasiasa watatoa kwa ajili ya kufadhili miradi katika makanisa yetu. Sio wajibu wetu kama kanisa kubaini walikotoa pesa hizo” kanisa hilo lilieleza katika taarifa mwezi Januari .

Isitoshe, mwezi jana Maaskofu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjilisti na ya Kiasili Nchini (FEICCK) walisisitiza kuwa wataendelea kupokea pesa za wanasiasa kwa sababu “hizo ni pesa za Mungu sio wanasiasa”.

Mhadhiri wa Somo la Dini ya Kikristo katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Andrew Kuria, anasema makanisa, hasa yaliyoanzishwa nchini baada ya uhuru, yanavutiwa na pesa sababu uwezo wao kifedha ni mdogo.

“Kando na kuwa waumini ni wachache, mengi hayana ufadhili wowote ikilinganishwa na makanisa makubwa. Pili, uchu wa pesa unachangiwa na mtindo wa nyakati hizi wa baadhi ya viongozi wa makanisa kusawiri makanisa kama chanzo cha utajiri,” alisema mwezi jana.