Papa alizuru mataifa 68 lakini hakurudi kwao nyumbani Argentina
VATICAN CITY
KATIKA kipindi cha miaka 12 ya uongozi wake, Papa Francis alitembelea mataifa 68, akiongoza harakati za kueneza Neno la Mungu na upendo wa Mungu kwa binadamu wote bila kuchoka.
Kutoka Rio hadi Ajaccio, ziara zake 47 za Kitume zilimpeleka katika kila bara na karibu kila pembe ya dunia.
Ni safari moja tu, ambayo wengi waliisubiri lakini haikutimia: ziara ya Argentina, taifa alikozaliwa. Aliondoka kwenda Roma mwaka 2013 kwa mkutano wa kuchagua Papa, lakini hakuweza kurudi.
Tangu ziara yake mwaka 2013 kuelekea Brazil, picha ya Papa Francis akiwa amebeba mfuko wake mdogo mweusi alipokuwa akipanda ndege ilivutia dunia.
Wakati wa safari hiyo, alitembea ndani ya ndege, akisalimiana na wanahabari kwa urafiki na kujenga mahusiano ya kawaida yasiyo na ubaguzi wa vyeo.
Alipotua nchini humo, alikataa kutumia gari la kivita lililoambatana na ulinzi mkali, na badala yake, alipendelea kutumia magari ya kawaida au magari ya wazi, ili aweze kuungana na watu, kushiriki maisha yao na kuhisi hisia zao.
Hakuanza ziara yake ya kimataifa katika taifa kubwa, bali kisiwa cha Lampedusa – lango la Ulaya kwa maelfu ya wahamiaji waliokuwa wakikimbia vita, mabadiliko ya tabianchi na umaskini.
Ziara hiyo ilikuwa ishara wazi kwamba uongozi wake ungejikita kwa watu waliosahaulika – maskini, wahamiaji, na waliotengwa.
Kupitia safari hizo, Papa alieleza wazi kuwa Kanisa lazima lisikie kilio cha walio dhaifu, waliopuuzwa na waliokata tamaa.
Alifanya wastani wa safari nne kila mwaka, akitumia kila ziara kuhimiza haki, amani, ujumuishaji na upendo kwa binadamu wote.
Japo afya yake ilianza kumlemea, hadi kulazimika kutumia kiti cha magurudumu na kughairi baadhi ya safari – sauti yake haikuwahi kufifia.
Hata Ulaya, bara linaloendelea kupoteza misingi yake ya kiroho, halikusahaulika.
Alitembelea Ubelgiji, akahimiza majadiliano kuhusu masuala magumu kama vile jinsia, mimba, na unyanyasaji wa kijinsia kanisani – akisisitiza kuwa hata mataifa tajiri yana “pembe za mateso” zinazohitaji upendo wa mchungaji mwema.
Safari zake nyingi zilikuwa hija za amani na upatanisho – akihimiza wanasiasa kuweka kando maslahi ya kibinafsi na kulenga ustawi wa wananchi wao.
Alitembelea mataifa kama Colombia, Sudan Kusini, Iraq na Canada, akiweka wazi kuwa hakuna kundi linalopaswa kutengwa.