Bado tunatishwa, tuwekeni kwa maombi, Jaji Koome asihi Kanisa
JAJI Mkuu Martha Koome ameomba Kanisa kuwa makini zaidi na kuendelea kuwa sauti ya kutetea taasisi huru dhidi ya vitisho.
Jaji Mkuu alisema kuwa Mahakama, kama vile mihimili mingine ya serikali, inapitia kipindi ambacho Wakenya hawathamini tena taasisi za kikatiba.
Jaji Mkuu na Majaji wa Mahakama ya Juu wanakabiliwa na kesi tatu za kuondolewa ofisini zilizowasilishwa mbele ya Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC).
Hata hivyo, Mahakama Kuu ilizuia JSC kuendelea na kesi hizo.
Akizungumza Alhamisi huko Meru wakati wa Mkutano wa Kamati ya Utawala ya Kanisa la Presbyterian Church of East Africa (PCEA), Jaji Koome alisema kuwa Mahakama haitazimwa na vitisho vyovyote.
“Tupo ili kulinda na kudumisha katiba. Wakenya walitoa nguvu zao za juu kwa mahakama kama ilivyoainishwa kwenye katiba. Kuna haja kwa Kanisa kuendelea kusimama imara katika kutetea taasisi huru hasa wakati zinapojaribiwa na kutishiwa,” alisema.
Jaji Mkuu aliongeza, “Ustawi na maendeleo ya demokrasia yetu unategemea uvumilivu na uaminifu wa taasisi huru kama vile Mahakama. Tupo ili kudumisha utawala wa sheria na kuhakikisha usawa na uwajibikaji.”
Jaji Mkuu alisema kuwa Kanisa linapaswa kutumia mamlaka yake ya kiroho kutetea na kuimarisha taasisi huru kama ilivyoainishwa katika katiba.
Aliongeza kuwa Mahakama itaendelea kushirikiana na Kanisa katika kukuza mfumo wa haki unaozingatia watu na unaoweza kufikiwa.
Jaji Koome alisema kuwa haki lazima iwe uzoefu wa kila siku ambapo inapatikana katika jamii.
“Tunafuata mbinu ambayo inatambua na kuunganisha mifumo ya kutatua migogoro kwa njia mbadala na mifumo ya haki ya jadi,” alisema.
Alitoa mfano wa matumizi ya upatanishi kutatua migogoro ya kisiasa tangu ghasia za uchaguzi za 2007.
Alirai Kanisa kushawishi taifa kuepuka kutumia vurugu kutatua mizozo ya kisiasa.
“Baada ya ghasia za 2007, tuliketi kwenye meza tukakubaliana na serikali ya mseto ikaundwa. Mwaka 2017, tulikuwa na migogoro kuhusu uchaguzi na tukawa na handisheki. Baada ya uchaguzi wa 2022, tulikuwa na migogoro na maandamano yaliyosababisha mauaji. Hatimaye tuliketi kwa meza na kukubaliana na tuko na Serikali Jumuishi. Kwa nini tusianze na mazungumzo badala ya kutumia vurugu?” Jaji Koome alihoji.
Kadhalika, alihimiza Kanisa kuhamasisha nchi kuhusu umuhimu wa kukumbatia mazungumzo kutatua migogoro ili kupunguza kesi mahakamami.
“Sielewi kamwe kwa nini familia zinapelekana mahakamani. Hata watoto wanawapeleka mama zao mahakamani kwa masuala ya urithi. Katika baadhi ya kesi, watu huenda mahakamani kuchelewesha na kuzuia haki kwa kutafuta tafsiri za kisheria. Tuunde umoja katika familia na tuzungumze na kila mmoja,” alisema.
Jaji Koome alitoa wito kwa makanisa na mashirika mengine ya kidini kutatua masuala yanayofikisha mahakamani.