Raila: Sauti ya Nyong’o, Orengo ni yangu
KINARA wa upinzani, Raila Odinga jana aliwatetea magavana James Orengo (Siaya) na Prof Anyang’ Nyongó (Kisumu) ambao wamekuwa wakikashifiwa kwa kukosoa utawala wa Rais William Ruto, akisema wanazungumza kwa niaba yake na chama cha ODM.
Bw Odinga alisema kuwa wawili hao hawafai kusulubishwa kwa kukosoa serikali, akisema wanasema ukweli na masuala waliyoyaibua yanahusiana na ugatuzi na lazima yatiliwe manani na serikali hii.
“Orengo hajafanya kosa lolote la kiuhalifu na ana haki ya kuzungumza kwa sababu tuko katika taifa la kidemokrasia. Hakuna makosa akizungumza kuhusu maelewano na ushirikiano wetu na UDA,
“Profesa Nyongó akiongea kuhusu ugatuzi anaongea kwa niaba ya ODM. Ugatuzi ndio muhimu zaidi katika katiba hii ambayo tuliandaa katika ukumbi wa Bomas,” akasema waziri huyo mkuu wa zamani
Alikuwa akizungumza wakati wa mazishi katika Kaunti ya Homa Bay ambako aliandamana na vigogo wa ODM akiwemo mwenyekiti wa chama Gladys Wanga.
Kigogo huyo wa siasa za upinzani, alisema kuwa Kenya ni taifa la kidemokrasia na kwa kuzindua ushirikiano na Rais Ruto, hakumaanishi kuwa hawawezi kukosoa serikali au kuzungumza serikali inapokosea kisera.
“Hatuna muungano wa kisiasa na UDA bali tuna ushirikiano nao ambapo baadhi ya wanachama wetu wanahudumu serikali na maelewano tuliotia saini hayamaanishi sisi sote tumeingia kwa serikali,” akaongeza.
“Watu wasipige kelele eti Raila alisema hii na mtu mwingine amekataa kufuata. Hakuna mgongano wowote ambao unastahili kutokea serikali ikikosolewa,” akasema.
Gavana Orengo amekuwa akikosolewa kutokana na matamshi ambayo alitoa mbele ya Rais Ruto na Bw Odinga eneobunge la Rarieda mnamo Aprili 12.
Wakati wa mazishi ya msaidizi wa kibinfasi wa Raila marehemu George Oduor, Bw Orengo alisema hawezi kuwa kibaraka kwa kuwa maendeleo ni haki ya raia wala hawafai kuipokea kutokana na hisani ya serikali.
“Mimi siwezi kuwa kibaraka kwa sababu tulipigania katiba ambayo watu wanaruhusiwa kuzungumza. Nilikuwa bunge ambalo wabunge walikuwa wakimwaambia Rais Daniel Moi kuwa hakuna mahali ataenda na angeongoza milele,” akasema Bw Orengo.
“Mkiendelea kuwa vibaraka hatutakuwa na nchi. Waambieni viongozi wenu ukweli na mimi siimbi mtu kwa sababu lugha ambayo nimesikia hapa, inaashiria kuwa nchi hii inapoteza hadhi yake,” akasema Bw Orengo
Gavana huyo alikashifiwa na baadhi ya viongozi wakuu wa ODM huku wale wa mashinani Nyanza wakipendekeza madiwani wa Kaunti ya Siaya wamtimue kwa kumpinga Raila.
Mnamo Jumatano, Profesa Nyongó naye alikuja juu juu na kurukia serikali ya Rais Ruto kuhusu kukwamilia fedha za ujenzi wa barabara akisema pesa hizo zinastahili kuwasilishwa kwa kaunti.
Profesa Nyongó alisema kaunti zinasimamia vyema sekta ya afya kwa hivyo itamudu hata kusimamia ujenzi wa barabara.
“Hatufai kukubali utawala huu uturejeshe nyuma na hatufai kuruhusu matunda ya mfumo wa ukombozi wa pili yapotee tu,” akasema Profesa Nyongó.
Kujitokeza hadharani kwa Raila kutetea Profesa Nyongó na Orengo kunatarajiwa kutuliza shinikizo ambazo zimekuwa zikiwaandama.
Baadhi ya viongozi wamekuwa wakidai wanatumiwa kuyumbisha serikali na kuwataka wakome ili eneo la Nyanza linufaikie kupitia miradi ya maendeleo
Baadhi ya wabunge wa ODM kama wa Homa Bay mjini Peter Kaluma, wamekuwa mstari wa mbele kumpapura Bw Orengo ambaye alipinga hatua ya ODM kujiunga na Rais Ruto katika kilele cha maandamano ya Gen Z mnamo Juni/Julai mwaka uliopita.
Jana, Bw Odinga aliwaambia wafuasi wake wakae ange akisema kuwa mbele ni kuzuri wala hajazama kisiasa.
“Simameni nami na tuwe pamoja na hapa mbeleni tutafika mahali ambayo tumekuwa tukilenga,” akasema kauli inayoweza kufasiriwa kuwa huenda akawania urais tena.
Raila aliunga mkono msimamo wa Profesa Nyongó kuhusu fedha za ujenzi wa barabara akisema hela ambazo zinastahili kugharimia maendeleo, hazitolewi na serikali kuu.
Kwa mara nyingine, alisisitiza kuwa Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (CDF) lazima iondolewe mikononi mwa wabunge ili pesa hizo zipewe kaunti kufanyia maendeleo.