Zaidi ya watu 25,000 wakosa kuchukua vitambulisho Mlima Kenya
MAAFISA wa utawala eneo la Mlima Kenya wamewataka watu waliotuma maombi ya vitambulisho vya kitaifa wavichukue katika vituo vya Huduma Centre eneo hilo.
Zaidi ya watu 25, 000 walioomba stakabadhi hizo hawajazichukua huku viongozi wa kisiasa nao wakiwataka vijana kuzichukua ili wajisajili kuwa wapiga kura.
Katika Kaunti ya Murang’a, zaidi ya vitambulisho 13, 000 havijachukuliwa na wenyewe, watu 6,000 kati yao wakiwa wale waliotuma maombi kwa mara ya kwanza.
Kulingana na msajili wa watu katika kaunti hiyo, Bi Juliet Mutitu, vingine ni vya watu wanaochukua vitambulisho vipya baada ya kupoteza vile vya zamani au kuharibika.
Afisa wa Vijana, Michezo na Utamaduni, Bw Noah Chachucha, alisema idara yake inashirikiana na maafisa wa utawala katika kutoa uhamasisho kwa wenye stakabadhi hizo ambazo hazijachukuliwa.
“Tunapitia wakati mgumu kuendesha mipango wa uwezeshaji kwa sababu vijana wengi waliotimu umri stahiki hawana vitambulisho ilhali stakabadhi hiyo zimerundikana katika vituo vya usajili,” Bw Gachucha akasema.
Huku kukiwa na zaidi ya vitambulisho 3,000 katika Huduma Centre mjini Nyeri, katika kaunti jirani ya Kirinyaga angalau vitambulisho 10, 000 havijachukuliwa.
Naibu Kamishna wa kaunti Joseph Mureithi alihoji jinsi wenye vitambulisho hivyo wanatarajia kushiriki katika uchaguzi au kusaka ajira bila stakabadhi hizo muhimu.
Aliwataka watu kama hao kutembelea Huduma Centre mjini Kerugoya na afisi zingine za usajili watu wakachukue stakabadhi hizo.
Akiongea katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kamuiru katika Eneo Bunge la Kirinyaga ya Kati wakati wa hafla ya utoaji wa hundi za basari za thamani ya Sh60 milioni kutoka Hazina ya Ustawi wa Eneo bunge hilo, mbunge wa eneo hilo Gachoki Gitari pia aliwataka vijana wote waliotimu umri wa miaka 18 kwenda juu kuwasilisha ombi la vitambulisho.
Katika kaunti ya Laikipia, jumla ya vitambulisho 2, 313 vya kitaifa vimerundikana katika vituo viwili vya Huduma Centre. Baadhi ya stakabadhi hizo ziliwasilishwa katika afisi hizo miaka minne iliyopita.
Idadi kubwa ya vitambulisho katika vituo vya Huduma Centre vya Nanyuki na Makutano, ambavyo havijachukuliwa na wenyewe ni vya wanaume (1,374) ilhali vingine (939) vikiwa vya wanawake.
Afisa mmoja katika Afisi ya Usajili wa Watu mjini Nanyuki Duncan Murage alisema stakabadhi hizi ni za watu waliozipoteza na kutuma maombi mapya lakini hawakurejea kuvichukua baada ya kuwa tayari.
Aidha, kuna wale ambao walitaka maelezo yao yabadilishwe au kurekebishwa lakini hawakurejea kuzichukua.
“Tunazianisha kama “wenye waliotuma maombi” kwa sababu hawatafuti usajili kwa mara ya kwanza. Miongoni mwao ni wale waliopoteza vitambulisho vyao na wale wanaotaka maelezo kwenye stakabadhi zao yabadilishwe kwa sababu mbalimbali,” akasema Bw Murage.