Makala

Sababu za Turkana kuongoza kwa Malaria nchini

Na Leon Lidigu April 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI ya Turkana  sasa imechukua nafasi ya kwanza kama kaunti yenye mzigo mkubwa zaidi wa malaria nchini Kenya, kulingana na takwimu mpya kutoka kwa Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Malaria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Turkana imebadilika kutoka kuwa eneo la milipuko ya msimu hadi kuwa eneo la malaria ya kudumu, na visa vya ugonjwa huo vimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 65 wakati wa misimu ya mvua tangu mwaka wa 2017.

Kwa kiwango cha maambukizi cha asilimia 39 kilichorekodiwa mwaka uliopita—ambacho ni mara sita zaidi ya wastani wa kitaifa wa asilimia 6—kaunti hiyo sasa imeorodheshwa kuwa eneo lenye mzigo mkubwa wa malaria chini ya Mkakati wa Kitaifa wa Malaria.

Katibu katika Idara ya Afya ya Umma na Viwango vya Kitaalamu, Bi Mary Muthoni, alieleza kuwa mvua kubwa inayonyesha Turkana huwafanya wakazi wengi kuwahifadhi wagonjwa nyumbani kutokana na hali mbaya ya hewa, hali inayotishia maisha.

Mwaka wa 2017, Turkana ilishuhudia mlipuko mbaya zaidi ambapo zaidi ya watu 45,000 walipatikana na maambukizi ya malaria ndani ya mwezi mmoja pekee. Eneo la Turkana Magharibi lilirekodi asilimia 65 ya visa hivyo.

Bi Muthoni alisema hali hii mpya imeifanya Turkana kuwa eneo muhimu la kuanzisha mkakati wa kudhibiti malaria kwa watoto wa umri mdogo kupitia mpango wa Seasonal Malaria Chemoprevention (SMC)—ambapo dawa za kuzuia malaria hutolewa kila mwezi wakati wa msimu wa maambukizi.

Katika mwaka wa 2024, awamu ya kwanza ya mpango huo ililenga eneo la Turkana ya Kati ambalo lilikuwa na visa 102,000 vya malaria, huku asilimia 60 ya maambukizi hayo yakitokea kati ya Mei na Septemba.

Mpango wa SMC ulizinduliwa mwezi Juni 2024 kwa msaada wa Catholic Relief Services (CRS) na unahusisha utoaji wa dawa aina ya sulfadoxine-pyrimethamine pamoja na amodiaquine (SP+AQ) kwa watoto walio chini ya miaka mitano. Dawa hizo hutolewa mlango kwa mlango na wasambazaji wa kujitolea wa jamii.

Bi Muthoni aliongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanachangia ongezeko la malaria Turkana kwa kuongeza maeneo ya maji yaliyosimama, ambayo ni mbu wanaoeneza ugonjwa huo huzaana.

Utafiti wa hivi karibuni kutoka Chuo Kikuu cha Georgetown nchini Amerika unaonyesha kuwa malaria imekuwa ikisambaa hadi maeneo ya juu zaidi barani Afrika kila mwaka kutokana na ongezeko la joto.

Kutokana na hali hiyo, mwaka 2012, WHO ilipendekeza SMC kama njia bora ya kuzuia malaria kwa watoto katika maeneo yenye milipuko ya msimu.

Mwaka jana, watoto 38,585 walio chini ya miaka mitano walipewa dawa hizo katika mizunguko mitano tofauti. Asilimia 71 (27,206) ya watoto hao walikamilisha mizunguko yote mitano ya tiba hiyo.