Utata wazuka kuhusu mazishi ya msichana aliyeuawa na simba
MVUTANO unatokota kati ya mama na baba ya msichana mwenye umri wa miaka 13 aliyeuawa na simba jike siku 10 zilizopita katika Kaunti ya Kajiado.
Mzozo kati ya mama huyo na mumewe waliyetengana (babake marehemu) unahusu mipango ya mazishi.
Msichana Peace Mwende, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Gredi ya 8 katika Shule ya Msingi ya Oloosirkon alishambuliwa na kuuawa na simba jike katika kijiji cha Tuala, Kaunti Ndogo ya Kajiado Mashariki.
Mamake, Bi Elizabethi Mawai, 46, aliambia Taifa Leo kwamba kifungua mimba wake alikuwa amemtembelea babake mahala pake pa kazi mnamo Alhamisi Aprili 17, 2025, siku nne baada ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.
Mwanamume huyo anafanya kazi katika ranchi inayopakana na Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi.
Hata hivyo, sasa Bi Mawai anapinga pendekezo la mwanamume huyo kwamba mtoto huyo azikwe nyumbani kwao (baba), katika Kaunti ya Nandi.
Taifa Leo ilipomtembelea mama huyo katika kijiji cha Tuala Jumanne, Aprili 29, 2025 anakoishi na watoto wake watatu, alikuwa amepoteza matumaini huku akionekana mchovu.
Bi Mawai na watoto wake wamekuwa wakiishi katika jengo lililochakaa, lililotelekezwa na mwenyewe kabla ya ardhi ambako lilijengwa kugawanywa kama ploti.
Mama huyo anaishi kwa umasikini wa kupindukia huku akiwa hana choo ishara kwamba yeye na wanawe wanaenda haja msituni.
Bi Mawia hujikimu kimaisha kwa kufanya vibarua katika maeneo ya karibu.
“Nimekuwa nikipokea vitisho kutoka kwa mpenzi wangu wa zamani akitaka kumzika binti yangu nyumbani kwao katika Kaunti ya Nandi. Alinitelekeza baada ya kupata ujauzito miaka 13 iliyopita. Nimevunjwa moyo,” akaelezea huku akitokwa na machozi.