Handisheki ya Uhuru, Gachagua sasa yabisha hodi
RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo Jumanne, Aprili 29, 2025 walionekana kuzika tofauti zao za kisiasa ili kuunda muungano wa kumpinga Rais William Ruto kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Hii ilikuwa baada ya, Dkt Fred Matiang’i, kukutana na Bw Gachagua katika hoteli moja jijini Nairobi pamoja na viongozi wengine wa upinzani kusuka muungano wa kumenyana na Dkt Ruto.
Jubilee inayoongozwa na Kenyatta imevumisha Dkt Matiangi kama mgombea urais wake.
Bw Gachagua alisema huo ulikuwa mkutano wa timu ya kukomboa Kenya unaokua kila siku.
“Karibu sana Dkt Matiang’i, uko upande sahihi wa historia,” naibu rais huyo wa zamani alisema.
Hii ilikuwa mara ya pili kwa Dkt Matiang’i kukutana na Bw Gachagua ndani ya siku nne, baada ya kukutana Jumamosi iliyopita, jambo lililoongeza hisia kuwa Bw Kenyatta hatimaye anamkubali Bw Gachagua kuwa mshirika kuelekea 2027.
Mkutano huo, pia, ulihudhuriwa na kiongozi wa chama cha Wiper Bw Kalonzo Musyoka, kiongozi wa chama cha DAP-K Bw Eugene Wamalwa, na kiongozi wa People’s Liberation Party Bi Martha Karua.
Wengine waliohudhuria ni aliyekuwa Waziri wa Huduma za Umma Bw Justin Muturi, aliyekuwa Waziri wa Kilimo Bw Mithika Linturi, Dkt Mukhisa Kituyi na mwanasiasa kutoka Bonde la Ufa, Bw Torome Saitoti.
Bi Karua alisema: “Ilikuwa asubuhi njema sana. Hii ndiyo timu itakayoikomboa Kenya.”
Naye Bw Musyoka alisema, “Hatua moja kwa wakati kuelekea lengo kuu la kuikomboa nchi.”
Katibu Mkuu wa Jubilee Bw Jeremiah Kioni aliambia Taifa Leo kuwa “hakufai kuwa na shaka. Rais wetu wa zamani anasimama imara upande wa wananchi na malengo ya haki kwa wote ndiyo anayotetea hadharani na faraghani.”
Bw Kioni alisema, “haijalishi nani atakasirishwa na maneno ya busara ya Bw Kenyatta, yeye si mtu wa kusema mambo ili kuridhisha watu wasiofaa, na wanajua hilo kwani walifanya naye kazi kwa miaka zaidi ya 30.”
Mchambuzi wa siasa Bw John Okumu, alitaja mkutano huo kama, “hatua ya mwanzo kabisa ya muungano wa kumpinga Ruto, ni kuungana kwa vigogo wa Mlima Kenya wanaodhibiti kura za jamii hiyo, na ni onyo kuwa mwaka wa 2027 hautakuwa rahisi kwa aliye madarakani.”
Wakati huo huo, mchanganuzi wa siasa, Bw Charles Mwangi, alisema mkutano huo “ulilenga kutangaza kuwa Dkt Matiang’i sasa ni mshirika, na kuonyesha kuwa Bw Kenyatta hatimaye anajiunga na mwelekeo wa wapigakura wa Mlima Kenya 2027.”
Bw Mwangi alisema uwepo wa Matiang’i katika mkutano wa Bw Gachagua ni ishara wazi kuwa Bw Kenyatta ameamua kushiriki kikamilifu katika juhudi za kumzuia Dkt Ruto kuchaguliwa tena na si habari njema kwa rais aliye madarakani.”
Baada ya takribani miaka minane ya vita vya kisiasa kati ya vigogo hawa wa siasa za Mlima Kenya, inaonekana sasa Bw Kenyatta na Bw Gachagua wanaungana kwa lengo la kumtoa Ruto madarakani.
Bw Gachagua aliwahi kuwa msaidizi wa kibinafsi wa Bw Kenyatta mnamo 1992 hadi 2013, Bw Kenyatta alipochaguliwa kuwa Rais wa Nne.
Baadaye Bw Gachagua aligombea ubunge wa Mathira mwaka 2017 na akashinda, lakini walitofautiana na Bw Kenyatta mwaka mmoja baadaye kuhusu azma ya urais ya Dkt Ruto.
Bw Gachagua aliungana na viongozi wengine wa Mlima Kenya kumpinga Bw Kenyatta, akiwemo Bi Jayne Kihara, Bi Alice Wahome, Bw Kimani Ichung’wah, Bw Ndindi Nyoro na Bw Moses Kuria.
Walifanikiwa, na Dkt Ruto alipata asilimia 87 ya kura za Mlima Kenya.
Bw Gachagua alihudumu kama Naibu Rais lakini baada ya miaka miwili, alitengwa na Rais Ruto ambaye alidhamini mchakato wa kumuondoa madarakani Oktoba mwaka jana, 2024.
Badala ya kusalimu amri, Bw Gachagua alijitokeza upya kama sauti kuu ya upinzani dhidi ya serikali ya Dkt Ruto, na sasa anaonekana kuunda muungano wa kumpinga.