Habari Mseto

Chokoraa waliosafirishwa Baringo warejeshwa Nakuru

February 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

WAKAZI wa eneo la Sawich, kaunti ya Baringo walipigwa na butwaa walipoamka na kupata kikundi cha watoto 41 wa kurandaranda mitaani katika kituo cha kibiashara Alhamisi, wakidaiwa kuwa walisafirishwa kwa nguvu kutoka mjini Nakuru.

Kisa hicho cha kushangaza kiliwaghadhabisha wakazi na viongozi wa kaunti ya Baringo, na kuwafanya kuwarejesha chokoraa hao, japo tayari walikuwa wamelala kaunti hiyo usiku kucha.

Alhamisi, seneta wa Nakuru Susan Kihika alikashifu serikali ya kaunti yake ambayo alidai kuwa maafisa wake ndio waliwafanyia watoto hao kitendo hicho, akimtaka Gavana Lee Kinyanjui kujitokeza kueleza sababu.

Baadhi ya chokoraa waliosafirishwa kwa nguvu kutoka mjini Nakuru. Picha/ Eric Matara

Bi Kihika alitaja kisa hicho kuwa cha aibu kwa kaunti hiyo.

“Gavana Kinyanjui ajitokeze na kueleza kuhusu kisa hiki. Waliofanya hivi sharti wakumbane na sheria. Nashangaa nini kingewatendekea watoto hao ikiwa wakazi wa Baringo hawangejitolea kuwaokoa,” akasema Bi Kihika.

Seneta huyo alisema kuwa maafisa kutoka afisi yake walisafiri hadi mjini Eldama Ravine na kuhakikisha kuwa watoto hao, mdogo akiwa wa miaka 10 walikuwa wakirejeshwa Nakuru.

“Lakini kwa bahati mbaya, watano kati ya watoto hao 41 walikuwa wakikosekana hadi wakati walipoondoka Eldama Ravine,” akasema, akiongeza kuwa mmoja wao alipatikana baadaye.