Raia wa Ubelgiji waliojaribu kuhepesha siafu 5,000 wasema walikuwa wanajifurahisha tu
RAIA wawili wa Ubelgiji ambao Jumatano walipigwa faini ya Sh1 milioni kwa kupatikana na siafu hai 5,000 ambao thamani yao ni Sh124 milioni, walidai waliwakusanya wadudu hao kujifurahisha tu.
Lornoy David na Seppe Lodewijckx walihukumiwa pamoja na raia wa Vietnam, Duh Hung Nguyen ambaye alikuwa ajenti wa kusafirisha mizigo kwa watu wanaoishi ngámbo ambao hawajatambuliwa.
Pia Mkenya Dennis Ngángá ambaye alikuwa broka katika biashara hiyo kutokana na ufahamu wake wa siafu alikamatwa.
Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) lilisema kuwa thamani ya kifedha ya wadudu hao ilikuwa Sh1.2 milioni japo utafiti uliofanywa na korti uliweka idadi hiyo kuwa Sh124.3 milioni.
Lornoy na Seppe walisema waliondoka Ubelgiji mnamo Machi, wakasafiri hadi Naivasha kutazama Mbio za magari za Safari Rally kisha wakawakusanya siafu hao bila kufahamu ni kinyume cha sheria za nchi.
Hata hivyo, hakimu mkuu aliyehusika na kesi hiyo alitilia shaka madai hayo.
“Kama lilikuwa jambo la kufurahia na kupenda mngewachukua wawili au watatu wa kike au hata kati ya tano-10 kufidia wale ambao wangekufa. Hakuna utetezi wa kuridhisha wa kupatikana na siafu 5,000,” akasema hakimu.
Aliwatoza faini ya Sh1 milioni kila moja la sivyo, watumikie kifungo cha mwaka moja gerezani.
Walipatikana wakiwa na wadudu hao Aprili 5, 2025 kwenye eneo la Lake View, Naivasha.
Wadudu hao walikuwa wamewekwa kwenye chupa ndogo 2,224 na kwa mujibu wa KWS, hatua hii ilikuwa ikilenga kuhakikisha wanaishi kwa miezi miwili zaidi.