Namatsi naye ajitosa kinyang’anyiro cha ubunge Butula 2027
SIASA za 2027 zimeanza kushika kasi katika eneobunge la Butula, Kaunti ya Busia huku miundomsingi, elimu na uwazi kwenye matumizi ya pesa zikiwa kati ya masuala ambayo wawaniaji wanatumia kujipigia debe.
Kushika kasi kwa kampeni kumetokana na hali kwamba Mbunge wa sasa Joseph Oyula aliyechaguliwa kwa tikiti ya ODM hajaweka wazi iwapo atatetea wadhifa wake au la.
Kimya chake kuhusu hatima yake kinaonekana kusababisha wawaniaji wengine wajitokeze kutoana kijasho.
Mwanasiasa Timothy Namatsi ni wa hivi punde kujitosa kwenye kinyángányiro cha ubunge akiahidi kuzamia miradi mbalimbali ya maendeleo kuliinua eneo hilo kiuchumi
“Butula inahitaji mwanasiasa anayewatumikia raia na kuwasikiza. Hatuwezi kuendelea kuwachagua viongozi wale wale na kutarajia maendeleo,” akasema Bw Namatsi.
Alikuwa akiwahutubia umma katika eneo la Marachi Magharibi ambako aliahidi makundi ya vijana na wanawake kuwa akichaguliwa atawekeza katika miradi ya kuwainua.
“Vijana wetu wanahitaji ujuzi, wanawake wetu nao wanahitaji mtaji, nitahakikisha wanayapata hayo yote. Pia tuna vijana wadogo werevu Butula ambao wanahitaji tu kupewa nafasi,” akasema huku akisisitiza kuwa elimu ataipa kipaumbele kwa kutumia Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (CDF) kuwalipia karo.
Katika kuimarisha miundomsingi analenga kujenga barabara ambazo zitawasaidia kufika shuleni, masoko na kwenye vituo vya afya. Haya yote analenga ili kufungua eneobunge hilo kustawi kiuchumi na kuimarisha maisha ya wakazi wake.
Mwanasiasa huyo alisema atakuwa akiandaa mikutano ya umma kila baada ya miezi mitatu akichaguliwa, kuwasikiza na kuhakikisha kuna uwazi kwenye matumizi ya pesa za CDF.
“Mikutano hii itakuwa ya kuhakikisha kuwa kilio cha raia kinasikizwa na mapendekezo yao yanatiliwa manani,” akaongeza.