Habari Mseto

Uhuru ataka mfumo mmoja wa ukusanyaji mapato na ushuru

February 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amezitaka Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), Baraza la Magavana Nchini (CoG) na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) kubuni mfumo wa pamoja wa ukusanyaji mapato na ushuru.

Alisema mfumo huo wa kidijitali unapasa kutumiwa na serikali zote 47 za kaunti kuimarisha viwango vya ukusanyaji mapato ya kufadhili huduma na miradi ya maendeleo mashinani.

“Naamuru CRA, CoG na KRA kufanya kazi kwa ushirikiano na jopo maalum shirikishi ili kubuni mfumo wa pamoja wa ukusanyaji mapato katika ngazi ya kitaifa na mashinani,” Rais Kenyatta akasema.

Rais alisema hayo jana katika jumba la KICC, Nairobi alipozindua rasmi Mpango wa Pamoja wa Kitaifa wa kutambua Rasilimali zilizoko Nchini (JNRM).

Mpango huo unaoendeshwa, kwa pamoja, na serikali ya kitaifa na zile za kaunti pia unahusu utayarishaji wa ramani mpya ambayo zitatumiwa kuandaa mipango ya maendeleo kote nchini.

Kenya imekuwa ikitumia ramani ambazo zilitayarishwa katika enzi za ukoloni ambazo haziafikiani na mahitaji ya kisasa.

“Ngazi zote mbili za serikali zimekuwa zikikabiliwa na changamoto katika ukusanyaji mapato kutoka na na ugumu ulioko katika utambuzi na ukaguzi wa rasilimali zilizoko nchini. Hii ni kwa sababu hatujakuwa na ramani sahihi,” akasema Rais Kenyatta.

Rais aliwapongeza wanachama wa jopo lililoendesha kazi hiyo, wengi wao wakiwa watalaamu wenye umri mdogo, kwa kufanya kazi nzuri na kwa gharama ya chini.

“Kazi hii ambayo ingetugharimu Sh140 milioni sasa imefanywa na vijana hawa wetu kwa gharama ya Sh700,000 pekee. Hongera kwao kwa kazi nzuri,” Rais Kenyatta akasema.

Mwenyekiti wa CoG Wycliffe Oparanya alipongeza mpango huo akisema utawezesha serikali za kaunti kutambua rasilimali zao na vianzo vya ukusanyaji ushuru.

“Kwa mfano, kwa kupenyeza mtambo wa tarakilishi, tutaweza kujua kampuni zote zilizoko katika kaunti tunazosimamia kando na rasilimali nyinginezo. Hii itatuwezesha kuimarisha viwango vyetu vya ukusanyaji mapato na kando na kupanga maendeleo,” akasema Bw Oparanya ambaye ni gavana wa Kakamega.

Magavana wengine waliohudhuria shughuli hiyo ni; Mwangi Wa Iria (Murang’a), Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Nderitu Murithi (Laikipia) na Anne Waiguru (Kirinyaga).

Naye Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru alisema wataalamu hao tayari wametayarisha ramani 75 za kidijitali za nchi nzima.

“Baadhi ya ramani hizi ndizo zitazisaidia serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuimarisha viwango vya ukusanyaji mapato na matumizi yazo,” akasema.

Akaongeza: “Ramani hizo zinatoa maelezo biashara zote na majumba ambayo yanapasa kulipiwa ada mbalimbali ikiwemo ile ya ardhi.”

Bw Mucheru alisisitiza kuwa kazi hiyo imefanywa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ICT ambayo itawezesha data kupatikana kwa urahisi.

Wizara zingine zilizoshirikishwa katika mpango huo ni; Ardhi, Ulinzi, Usalama wa Ndani, Kilimo na Fedha, ambazo zilitwasilisha wataalamu katika jopo lililoendesha kazi hiyo.