Habari Mseto

NMG, SG, KBC, Radio Africa na Capital zatisha kujiondoa kwa asasi ya utafiti

February 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

KAMPUNI tano kuu za habari nchini zinalalamikia Shirika la Utafiti kuhusu Umaarufu wa Vyombo vya Habari (KARF) kwa kutoa matokeo yasiyo sahihi kuhusu umaarufu wa vyombo vyake vya habari.

Kwenye barua zilizotuma kwa KARF, kampuni za; Nation Media Group (NMG), Standard Media Group (SG), Kenya Broadcasting Corporation (KBC), Radio Africa Group na Capital Group Limited, ziliipa makataa ya siku saba iondoe kutoka mtandao wake matokeo ya tafiti zake ilizochapisha miaka iliyopita na ikome kuchapisha matokeo ya tafiti zingine la sivyo zijiondoe na kusaka huduma hiyo kwingineko.

“Kutokana na udharura wa suala hili tunataka uchukue hatua tuliopendekeza kwa muda wa siku saba la sivyo tutaanza harakati za kutafuta asasi nyingi ambayo inaweza kutathmini hali katika sekta hii ya njia huru na itakayoaminika,” ikasema barua hiyo ambayo nakala yake ilitumwa kwa vyombo vya habari.

Wakuu wa mashirika hayo matano walisema kuwa utendakazi mbaya wa KAFR umeathiri mahusiano yao na wateja wao wa kununua nafasi za matangazo na maamuzi yao uchapishaji au upeperushaji habari.

Pia mashirika hayo yanaisuta KARF kwa kutumia mbinu za zamani kuendesha utafiti, hali inayotoa matokeo ambayo hayaakisi hali halisi, haswa usambazaji habari kwa njia ya digitali.

KARF hukusanya data kuhusu mienendo ya Wakenya ya kufuatilia habari katika vyombo mbalimbali kila siku siku kupitia mahojiano na watu 3,000. Wanaohojiwa huwakilisha watu ambao hufuatilia habari kupitia vyombo mbalimbali kama vile redio, runinga, magazeti na mitandaoni. Wanaohojiwa huwa ni wenye umri wa miaka 15 kwenda juu.

Kulingana na utafiti wa mwaka 2018, kati ya Wakenya 16 milioni ambao hufuatilia habari, asilimia 64.8 huthamini redio, asilimia 30.6 huthamini runinga na asilimia 1.6 hupendelea magazeti. Na ni asilimia 1.9 pekee hupendelea habari mitandaoni huku asilimia 0.8 wakipenda mitandao ya kijamii, wengine wakisoma majarida.