Gachagua azindua chama cha DCP huku genge likijaribu kutibua hafla
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua hatimaye amezindua chama chake kipya, Democracy for the Citizens Party (DCP), kama hatua ya kujiandaa kumenyena kisiasa na aliyekuwa mkubwa wake, Rais William Ruto wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Nembo ya chama kipya ni sikio linalosikiliza, na kauli mbiu yake ni “Skiza Wakenya”, ikiwa na rangi za kijani kibichi yenye mwangaza, nyekundu ya kutu, na nyeupe.
Bw Gachagua alijiteua kuwa kiongozi wa chama na akawatangaza kaimu maafisa watakaosimamia chama hicho kipya.
“Kama Kiongozi wa Chama cha Democracy for the Citizens Party, naahidi kwamba nitasikiliza watu wa Jamhuri ya Kenya na kutimiza matamanio yao,” alisema Bw Gachagua.
Uchambuzi wa majina yaliyotangazwa unaonyesha kuwa wengi wao ni wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi mkuu uliopita. Wengine ni watu wasiojulikana sana.
Baadhi ya washirika wa Bw Gachagua walichaguliwa kwa tiketi ya UDA na wako hatarini kufukuzwa kwa kujihusishwa waziwazi na chama kipya, jambo lililowafanya kuamua kutokubali nafasi za uongozi.
Katibu Mkuu wa zamani wa UDA, Cleophas Malala, ametajwa kuwa Kaimu Naibu Kiongozi wa chama, huku Hezron Obaga akihudumu kama Katibu Mkuu.
Martin Ole Kamwaro ametajwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Franklin Mithika Linturi atakuwa Katibu wa Kitaifa wa Mipangilio.
Peter Mwathi, aliyekuwa Mbunge wa Limuru, atahudumu kama Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa wa DCP anayesimamia mikakati. Mably Sarah Owino, mtu asiyefahamika sana, atahudumu kama Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa anayesimamia operesheni, na Annah Kavuu Mutua atakuwa Mweka Hazina wa Kitaifa.
Everngeline Wanjira Njoka na Thomas Mwita Nyangi wametajwa kuwa Manaibu Weka Hazina wa Kitaifa, wakisimamia mikakati na operesheni mtawalia.
Bi Cate Waruguru, aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake Laikipia atakuwa kaimu Kiongozi wa Wanawake wa Kitaifa; Serah Wanjiku Thiga, Kiongozi wa Vijana wa Kitaifa; John Maranga, Kiongozi wa Watu Wenye Ulemavu (PWD); Maina Kamanda, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Mashuhuri; na David Njenga Gikonyo, Kiongozi wa Baraza la Wakenya wanaoishi ng’ambo.
Wengine ni Abubakar Abdi Ogle (Naibu Katibu wa Kitaifa wa Mipangilio – Mikakati), Miriam Fredina Mariki (Naibu Katibu wa Kitaifa wa Mipangilio – Operesheni), Andrew Kiplimo Muge (Mkurugenzi wa Uchaguzi), Barnabas Kinyua Mpekethi (Kiongozi wa Kidini) na Brenda Banjira.
Bw Gachagua alieleza kuwa chama chake ni suluhisho kwa matatizo mengi yanayowakumba Wakenya, yakiwemo “mzigo wa ushuru, huduma mbovu za umma, gharama ya juu ya maisha, huduma duni za afya, sera mbaya, uongozi mbovu, ukosefu wa usalama na uongo wa kudumu, kati ya mengine.”
“Ujumbe wetu uko wazi: watu wa Kenya bado hawajamalizana nanyi. Tuna miadi nanyi Agosti 2027. Hatujasahau mliyoyafanya kwa uchumi wetu na kwa vijana wetu wa kiume na wa kike mwezi Juni 2024. Hatujasahau uongo mwingi na ahadi zisizotekelezeka mnazotupatia kila siku. Hatujasahau. Tutawakumbusha Agosti 2027,” alihitimisha.