Sudan Kusini yakemea vikali uvumi kwamba Rais Salva Kiir amefariki
JUBA, SUDAN KUSINI
WIZARA ya Masuala ya Kigeni na Uhusiano wa Ndani wa Sudan Kusini jana iilikanusha vikali kwamba Rais Salva Kiir Mayardit ameaga dunia.
Ilisema kuwa taarifa hizo zilikuwa uongo, za kutiliwa shaka na zilizolenga kuhakikisha taifa hilo changa zaidi Afrika, linakosa udhabiti.
Uvumi kuhusu kile kilichodaiwa kuwa mauti ya Kiir ulienea mno mitandaoni hasa wakati huu ambapo Sudan Kusini imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya kivita.
“Mheshimiwa Rais Salva Kiir Mayardit yu hai, ni mzima na anashughulika sana na masuala ya nchi. Anaendelea kuongoza akiwa imara kiafya,” Wizara ya Masuala ya Nje ya Sudan Kusini ikatoa taarifa.
Serikali hiyo iliwataka raia wa Sudan Kusini wapuuze uvumi huo waliousema unalenga kusababisha ukosefu wa amani na pia ukosefu wa udhabiti.
Utawala wa Juba pia ulishutumu wanaoeneza uvumi huo kama maadui wa amani ambao hawataki nchi hiyo ipige hatua kimaendeleo.
“Habari hizo feki zinalenga kukidhi tu nia ya watu ambao hawapendi amani ambayo Sudan Kusini inayo. Ni maadui wa amani, maendeleo, ujenzi wa taifa na udhabiti wa Sudan Kusini,” ikaongeza taarifa hiyo.
Hii ni mara ya nne ambapo uvumi kuhusu kifo cha Kiir umeenea.
Mei 20, kulikuwa na maswali kuhusu afya yake baada ya kukosa kuonekana hadharani kwa miezi kadhaa, ripoti zikidai alikuwa amepata virusi vya corona na akafariki.
Uvumi mwingine ulidai alikuwa amesafiri kuelekea Misri kutibiwa na kuachilia uongozi.
Mnamo Mei 25, 2020, Kiir alizungumza na taifa kupitia taarifa akikanusha uvumi huo na kusema alikuwa imara kiafya.
Pia kulikuwa na uvumi kuwa ameaga dunia mnamo Oktoba 2016 na Oktoba 2009.