Habari

Karua azimwa kuingia Tanzania kwenda kumtetea Tundu Lissu aliye korokoroni

Na CHARLES WASONGA May 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa chama cha People’s Liberation Party (PLP) Martha Karua amefichua kuwa amezuiliwa kuingia nchini Tanzania ambako alitarajiwa kumtetea kortini kiongozi wa upinzani Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uhaini.

Kwenye ujumbe kupitia akaunti yake ya mtandao wa X Jumapili asubuhi Mei 18, 2025, Bi Karua alisema kuwa yeye na watetezi wa haki za kibinadamu Lynn Ngugi na Gloria Kimani wanazuiliwa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salama huku maafisa wa serikali wakipanga kuwarejesha Kenya kwa nguvu.

Niliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere saa tatu na nusu asubuhi, na maafisa wa Idara ya Uhamiaji wakatwaa paspoti yangu na wakaipelekea wasimamizi wao ambao walituweka kwa muda huku wakishauriana na wakubwa wao — Martha Karua

“Msimamizi huyo sasa anatuambia kuwa tumezimwa kuingia Tanzania. Hakuna sababu iliyotolewa kwetu. Inanikera kwamba kama raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, nazuiliwa kuingia katika taifa mwanachama bila sababu maalum,” akaongeza akishangaa kuwa utawala wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan unaweza kumzuia kuingia Tanzania ilhali yeye sio tishio kwa usalama wa nchini hiyo.

Bi Karua, Bi Ngugi na Bi Kimani walikuwa sehemu ya ujumbe wa wanasheria na wanachama wa mashirika ya kijamii walioalikwa na Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), kwa ushirikishi wa Chama cha Mawakilishi Nchini (LSK) na kile cha mawakili wa Uganda (ULS).

Walikwenda Tanzania tayari kutetea kortini Bw Lissu anayeratibiwa kufikishwa kortini Jumatatu Mei 19, 2025, kujibu kosa la uhaini.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alikamatwa mwezi jana na kuzuiliwa korokoroni.

Idara ya Uhamiaji Tanzania haikuwa imetoa taarifa yoyote kuhusu kuzuiliwa kwa Bi Karua na wenzake, tulipokuwa tukiandaa ripoti hii.

Hata hivyo mawakili na watetezi wa haki wamekashifu kisa hicho na kuutaka utawala wa Rais Samia kuheshimu haki wa raia wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuingia nchini na haki ya mawakili kuwakilisha washtakiwa katika mataifa ya jumuiya hiyo.

Hii ni mara ya pili Bi Karua, ambaye ni wakili mtajika, kuwekewa vikwazo anapotaka kumwakilisha mwanasiasa kortini.

Mapema mwaka huu, aliwekewa viunzi alipofika Uganda kumwakilisha kiongozi wa upinzani Kizza Bessigye.