Ujasiri mkuu viongozi wa upinzani wakimponda Ruto kushoto, kulia
KADRI uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 unavyokaribia, ujasiri wa wananchi, viongozi wa kisiasa, na wanaharakati wa kijamii kuikosoa serikali ya Rais William Ruto unaonekana kuongezeka kwa kasi.
Huku ikibaki miaka miwili pekee kabla ya Wakenya kurejea kwenye debe, sera za serikali zinazidi kukosolewa hata na mahakama katika kile wachanganuzi wanasema ni changamoto kwa serikali ya Rais Ruto.
Licha ya waliokosoa serikali mwaka jana kulengwa na kutekwa nyara, wananchi wa kawaida kupitia mitandao ya kijamii, viongozi wa dini, wachambuzi wa siasa, na hata baadhi ya wabunge kutoka chama tawala wameanza kutoa maoni ya wazi kuhusu changamoto za kiuchumi, ahadi ambazo hazijatimizwa, na namna serikali inavyoshughulikia masuala ya wananchi.
Miongoni mwa masuala yanayozua ukosoaji mkubwa ni kupanda kwa gharama ya maisha, ushuru unaowakandamiza Wakenya na hisia kwamba baadhi ya miradi ya maendeleo haijaweka mbele maslahi ya mwananchi wa kawaida.
Aidha, kumekuwa na shutuma dhidi ya ongezeko la ukabila katika ajira za serikali na ubaguzi katika ugavi wa rasilimali.
“Inadhihirisha kuwa wananchi wameanza kutambua nguvu ya sauti yao na nafasi yao katika kuamua mustakabali wa nchi. Ikiwa inataka kurekebisha hali, serikali ya Ruto ni lazima isikilize kwa makini na kujibu hoja hizi kwa uwazi na mikakati madhubuti.
Ikiwa haitafanya hivyo, inaweza kujikuta kwenye nafasi ngumu sana katika uchaguzi wa 2027,” asema mchanganuzi wa siasa na utawala Bethwel Keino.
Aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, anaendelea kutumia maneno makali akikosoa serikali hasa baada ya kuzindua chama chake kipya cha kisiasa cha Democracy for Citizens Party (DCP) katika hafla iliyokumbwa na vurugu na madai ya kuingiliwa na ‘magenge ya kihalifu’ yanayodaiwa kutumwa na serikali.

Gachagua aliishutumu serikali ya Ruto kwa kutumia polisi na wahuni kuvuruga mikutano yake ya kisiasa, akitaja matukio kadhaa ya kushambuliwa kwake na familia yake, hata kwenye hafla za maombi.
Mnamo Alhamisi aliyekuwa Waziri wa Huduma za Umma na Mwanasheria Mkuu wa zamani, Justin Muturi, alimshambulia moja kwa moja Rais Ruto na kwa ujasiri, akamtaka ajiuzulu, akimlaumu kwa kusema uongo mara kwa mara na kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba.
Muturi pia aliwataka wabunge kutumia Ibara ya 145 ya Katiba kuanzisha mchakato wa kumuondoa Rais madarakani kwa tuhuma za ukiukaji wa haki za raia na utekaji nyara wa vijana wa Kenya, jambo ambalo anasema Ruto mwenyewe alikiri hadharani.
“Namshauri William Ruto afanye jambo la heshima — ajiuzulu. Hafai kuendelea kushikilia wadhifa huo, amekuwa mwongo asiyeweza kurekebishwa.”
“Ruto alikiri mwenyewe kuwa aliagiza vijana watekwe nyara. Hilo ni kosa la kikatiba. Bunge lina wajibu wa kuanzisha mchakato wa kumuondoa madarakani kwa kuzingatia Ibara ya 145,” Bw Muturi alisema.

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, naye amemshutumu Rais kwa kuvunja taratibu za kikatiba katika uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa IEBC.
Kalonzo alisema uteuzi huo ulikosa mashauriano ya kina, na ni dalili kwamba serikali inapanga kuiba kura katika uchaguzi ujao.
Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba, alizua gumzo baada ya kutuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akisema, “Wantam ni lazima” kauli ambayo imechukuliwa kama ishara ya kumuondoa Ruto madarakani baada ya muhula mmoja tu.
Wamuchomba, ambaye ni mshirika wa karibu wa Gachagua, ameendelea kujitokeza kuwa miongoni mwa viongozi wa Mlima Kenya wanaotofautiana waziwazi na serikali ya Kenya Kwanza.
Alikuwa miongoni mwa viongozi waliokataa kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2024 licha ya shinikizo kutoka kwa chama.
“Kufikia sasa, kuna dalili wazi kwamba ujasiri wa kuikosoa serikali ya Rais William Ruto umeongezeka, si tu kutoka kwa wanasiasa wa upinzani, bali pia kutoka kwa waliokuwa washirika wake wa karibu. Ikiwa serikali haitarekebisha mwelekeo wa utawala wake, basi uchaguzi wa 2027 unaweza kugeuka kuwa kura ya maamuzi kuhusu uhalali wake wa kisiasa,” asema Keino.
Mdadisi wa siasa Muli Koli asema ujasiri wa Wakenya kuponda serikali unaungwa mkono na mahakama ambayo imezima baadhi ya sera na mipango ya serikali.
Hali ya kisiasa inazidi kuwa tete huku viongozi waliokuwa ndani ya serikali wakiongoza harakati za upinzani.
Kauli zao si tu kwamba zinazidi, bali pia zinachochea ari ya upinzani kuelekea 2027. Kuna maamuzi ya mahakama yanayowapa viongozi na Wakenya nguvu kwa kuzima mipango na sera za Kenya Kwanza,” asema Koli.
Asema ikiwa mwenendo huu utaendelea, Rais Ruto atakabiliwa na ushindani mkubwa 2027.