Jamvi La Siasa

Malala ajivua kivuli cha Mudavadi, Wetang’ula

Na  BENSON MATHEKA May 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUREJEA kwa aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala katika uongozi wa chama cha kisiasa kupitia Democracy for the Citizens Party (DCP) kunaweza kuleta wimbi jipya katika siasa za Magharibi ya Kenya.

Malala, aliyekuwa Katibu Mkuu wa UDA, sasa ni Kaimu Naibu Kiongozi wa chama hicho kipya kinachohusishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Aliondolewa katika uongozi wa chama tawala kwa kile alichodai ni kumuunga mkono Bw Gachagua.

Wadadisi wanasema ukakamavu na ujasiri wa Bw Malala huenda ukabadilisha mwelekeo wa siasa za eneo la Magharibi ya Kenya hasa iwapo atafaulu kuvutia viongozi na wapigakura vijana.

Kurejea kwake kumejiri wakati ambapo viongozi vijana kutoka Magharibi – akiwemo Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya – wanaonyesha kutoridhika na uongozi wa kisiasa wa eneo hilo unaoshikiliwa na Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula na iwapo wanaweza kuunganisha nguvu zao, wanaweza kubadilisha siasa za eneo hilo, asema mdadidisi wa siasa Bwuuka Kisalo.

Chama cha DCP pia kinajiandaa kuwa sehemu ya vuguvugu la upinzani nchini, pamoja na vyama kama DAP-K kinachoongozwa na Eugene Wamalwa ambaye pia anatoka Magharibi. Wamalwa, tayari ameelekeza nguvu zake katika upande wa upinzani, na anaonekana kuwa mshirika wa karibu wa Malala katika kuunda nguvu mpya ya kisiasa Magharibi.

“Malala anaonekana kujiunga na kundi linalozidi kuongezeka la viongozi vijana wa eneo la Magharibi ambao wameanza kukosoa waziwazi mtindo wa uongozi wa Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula. Kundi hili linajumuisha viongozi kama Gavana Natembeya, ambao wamekuwa wakisisitiza haja ya kizazi kipya cha viongozi wanaojali maslahi ya eneo la Magharibi,” aeleza Kisalo.

Anasema ushirikiano kati ya Malala, Natembeya na Wamalwa unaweza kuunda wimbi jipya la upinzani ambalo linaweza kuwa tishio kwa uongozi wa Kenya Kwanza eneo la Magharibi.

“Viongozi walio serikalini kama Mudavadi na Wetang’ula watalazimika kujizatiti upya ili kulinda nafasi zao kisiasa dhidi ya wimbi la mabadiliko linalojiri,” asema mchanganuzi wa siasa James Maloba.

Huku DCP ikiendelea kujipanga kwa uzinduzi mkubwa Juni 5, 2025 ishara zote zinaonyesha kwamba siasa za Magharibi ziko kwenye njiapanda kwa kuwa halina msemaji mmoja wa kuliunganisha kama maeneo mengine.

“Ikiwa Malala ataungwa mkono na viongozi vijana na wapigakura vijana ambao ndio wengi, na ana ujasiri na uwezo, kuna uwezekano mkubwa wa mabadiliko makubwa ya kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2027 katika eneo la Magharibi,’ asema Maloba.

Wale wanaounga mkono Kenya Kwanza Magharibi mwa Kenya watalazimika kuchukua hatua tena kwa makini, la sivyo wasombwe na wimbi linalovuma nchini.

Kwa kujiunga na Gachagua, aeleza, Maloba, Malala anajenga nafasi ya kujiimarisha kama kiongozi anayekumbatia siasa za kitaifa na kujivua kivuli cha Musalia na Wetang’ula. Iwapo Malala ataweza kushawishi vijana, viongozi wa ngazi za kati, na wafuasi waliovunjika moyo na siasa za Kenya Kwanza, basi anaweza kutikisa mizani ya uongozi katika eneo la Magharibi.

Hatua hii inaweza kulazimisha Kenya Kwanza kubadili mbinu zake katika eneo hilo.Hata hivyo, Maloba asema changamoto kubwa kwa Malala na DCP itakuwa kudumisha mshikamano wa chama kipya, kujiepusha na migogoro ya ndani, na kushawishi wapigakura kuwa wao ni chaguo bora la uongozi mbadala.