Mahakama yaidhinisha ushindi wa Gavana Ndiritu Muriithi
Na RICHARD MUNGUTI
GAVANA wa Laikipia Ndiritu Muriithi ameibuka mshindi kwa mara ya tatu baada ya Mahakama ya Juu kutupilia mbali kesi ya kupinga uchaguzi wake iliyowasilishwa na aliyekuwa ajenti mkuu wa chama cha Jubilee Bw Sammy Ndung’u Waity.
Bw Muriithi aliungana na Mbunge wa Shinyalu Bw Justus Kizito Mugali kufurahia ushindi wao baada ya mahakama hii ya upeo kuwatangaza washindi halisi wa viti vyao.
Jaji Mkuu David Maraga na majaji Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang , Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na Isaac Lenaola walikubaliana na maamuzi ya mahakama za rufaa zilizotupilia mbali kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa Mabw Muriithi na Kizito.
Katika kesi ya Bw Muriithi majaji hao walisema Gavana huyo alishtakiwa na Bw Waity kwa kukihama chama cha Jubilee dakika za mwisho mwisho za mwaka wa 2017 baada ya kunyimwa fursa ya kuwania kiti hicho kwa tikiti ya Jubilee.
“Makosa ya Bw Muriithi yalikuwa alikihakama cha Jubilee na kujitosa kinyang’anyironi kama mwaniaji huru,” majaji hao wa mahakama ya juu walisema.
Bw Muriithi ndiye mwaniaji huru wa pekee katika kaunti 47 aliyeshinda uchaguzi huo akiwa mwaniaji huru.
Kutupiliwa mbali kwa rufaa ya Bw Waity katika mahakama hii ya upeo ilitia kikomo msururu wa kesi dhidi ya Bw Waity ambaye wafuasi wake walifanya maombi nje ya Mahakama ya Juu kumshukuru Mungu kwa kumtulizia kiongozi huyo machafuko na misukosuko ya kisiasa yaliyomwandama kwa muda mrefu.
Katika malalamishi yake Bw Waity alisema Bw Muriithi hakuwa ameteuliwa kwa njia ipasayo na angelizuiliwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kuwania kiti hicho alichokuwa anaking’ang’ania na Bw Joshua Irungu.
Majaji hao sita walisema katika uamuzi uliosomwa na Jaji Wanjala kwamba hakuna ushahidi uliowasilishwa mbele yao na Bw Waity ila makaririo ya tetezi zake katika Mahakama kuu na Mahakama ya Rufaa.
“Hakuna sababu hata moja iliyowasilishwa mbele yetu kututhibitishia tunapasa kubadili maamuzi ya wapiga kura wa kaunti ya Laikipia na kuharamisha ushindi wa Bw Muriithi,” walisema majaji hao.
Korti ilisema kile Bw Waity aliwasilisha ni mzozo wa utaratibu wa uteuzi ambao majaji walisema ulipasa kuamuliwa na jopo la kuamua IEBC la kutoa suluhu ya farakano za vyama vya kisiasa ama jopo ya kutatua kesi za wafuasi wa vyama vya kisiasa (PPDT).
“Bw Waity alitakiwa kujua akiwa ajenti mkuu wa Jubilee kwamba suluhu ya mzozo huo wa uteuzi ungeliamuliwa na IEBC au PPDT na wala sio mahakama,” alisema Jaji Wanjala aliposoma uamuzi huo kwa niaba ya wenzake.
Majaji hao walisema maamuzi ya mahakama za rufaa na kuu ni barabara na “ hawatavuruga uamuzi wa wapiga kura kumchagua Bw Muriithi kuwa gavana wao.”
Mahakama hiyo ilisema kuwa suala hilo halikupasa kufikishwa katika mahakama ya upeo kwa vile ilikuwa itatuliwe na majopo ya IEBC na PPDT.
Jaji Wanjala alisema kwa mahakama kuamua mzozo huo ni sawa na kutwaa mamlaka za majopo ya IEBC na PPDT ambazo zimepewa uwezo kamili kisheria kutoa suluhu kwa wasioridhika na uteuzi.
Wakati wa mvurugano huo wa uteuzi chama cha Jubilee kiliwasilisha malalamishi dhidi ya Bw Muriithi kwa jopo la IEBC.
Gavana huyo alitozwa faini ya Sh500,000 kwa kutumia picha za Rais Uhuru Kenyatta katika makaratasi yake ya kampeini akiwa mwaniaji huru.
Katika rufaa ya kupinga ushindi wa Bw Kizito mahakama ilisema mlalamishi ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa Shinyalu Bw Silverseter Lisamula Anami hakuthibitisha madai kwamba wapiga kura walihongwa na uchaguzi uliborongwa na IEBC ilipokaidi sheria za uchaguzi.
Bw Anami alikuwa amesema IEBC ilishindwa kuthibiti zoezi hilo la uchaguzi wa ubunge Shinyalu.
Mahakama hiyo Alhamisi ilithibitisha ushindi wa Gavana wa Homa Bay Bw Cyprian Awiti aliyeshtakiwa na mwaniaji huru Bw Oyugi Magwanga.
Rufaa ya kupinga uchaguzi wa Gavana wa Wajir Bw Ahmed Abdullahi.