Bonge la mgomo vyama 8 vya wahudumu wa afya vikitoa notisi
VYAMA vikuu vinane vya wafanyakazi wa afya nchini vimepatia serikali muda wa siku 14 kutimiza matakwa yao, vikionya kuwa kutakuwa na mgomo wa kitaifa iwapo wafanyakazi wa Mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) hawataajiriwa kwa ajira za kudumu na pensheni.
Muungano huo unawakilisha maafisa wa kliniki, wauguzi, wataalam wa dawa, wataalamu wa lishe, maafisa wa afya ya jamii, wahudumu wa mochari, na wataalamu wa maabara za matibabu, na akwa pamoja unashinikiza kuajiriwa kwa wahudumu walioajiriwa wakati wa mlipuko wa janga la COVID-19 mwaka 2020.
Viongozi wa vyama hivyo walisema kuwa makataa hiyo inatokana na hali ya kukata tamaa miongoni mwa wanachama wao kutokana na ahadi zisizotekelezwa na urasimu wa serikali ambao umewaacha maelfu ya wahudumu muhimu wa afya katika hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu ajira na marupurupu.
Tangazo hilo lilijiri kufuatia maandamano kadhaa ya wafanyakazi hao wakilalamikia masharti ya ajira na kutaka waajiriwe kazi ya kudumu na pensheni pamoja na kulipwa marupurupu ambayo wamekuwa wakiahidiwa kwa muda mrefu.
Wengi wao walipewa ajira za mkataba kwa ahadi kuwa nafasi hizo zitabadilishwa kuwa za kudumu. Hata hivyo, miaka imepita bila utekelezaji, huku wakilipwa mishahara ya chini hadi kwa asilimia 50 ikilinganisha na wenzao walio kwenye ajira za kudumu. Wanataka “mshahara sawa kwa kazi sawa.”
Wafanyakazi hao pia hawana usalama wa kazi, hawapati bima ya afya, pensheni, au fursa za kukuza taaluma – mambo ambayo kwa kawaida hutolewa kwa watumishi wa umma. Mbali na hayo, wamelalamika kuhusu unyanyasaji, ubaguzi, kunyimwa marupurupu na likizo, huku mgogoro ukiendelea kati ya serikali kuu na serikali za kaunti kuhusu nani anapaswa kuwaajiri na kuwalipa.
Katika kikao na waandishi wa habari Petterson Wachira Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Maafisa wa Utabibu Kenya na Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Afya, aliikemea serikali kwa kushindwa kushughulikia madai yao na kuwalaumu polisi kwa kutumia nguvu dhidi ya wafanyakazi wa UHC waliokuwa wakiandamana siku ya Jumanne.
“Tutaandikia Inspekta Jenerali wa Polisi na Mamlaka ya Kusimamia Polisi (IPOA) kuhusu ukatili wa polisi. Kama ndani ya siku 14 hatutapata ripoti ya hatua iliyochukuliwa dhidi ya maafisa waliowatendea unyama wanachama wetu, tutawashtaki. Na tutaita vyombo vyetu vya ushauri kuitisha mgomo wa kitaifa wa vyama vya afya,” alisema Wachira.
“Tunahitaji mikataba ya wahudumu wa afya wa UHC ibadilishwe kuwa ajira ya kudumu kuanzia Julai 1, 2025. Bajeti si jukumu letu, ni jukumu la Wizara ya Afya. Tunamtaka Inspekta Jenerali achukue hatua na aombe msamaha hadharani. Vinginevyo, tuko tayari kugoma,” aliongeza.
Bw Wachira alieleza kuwa mikataba ya muda mfupi inawazuia wafanyakazi kurudi shuleni kwa masomo ya juu au utaalamu, jambo linaloshusha ubora wa huduma wanazotoa.
“Inasikitisha kuwa serikali inayosema inatekeleza huduma ya afya kwa wote ndio hiyo hiyo inayowakandamiza wafanyakazi wake, haiwasaidii kuboresha ujuzi wao, na haiwalipi wanachostahili kulipwa,” alisema.
“Kwa suala la bajeti, serikali tayari imeweka pesa kwa ajili ya kulipa wafanyakazi wa mkataba kwa mwaka mzima. Wanaweza kutumia pesa hizo hizo kwa mishahara yao, kisha wafanye bajeti ya nyongeza ndani ya miezi sita kupata pesa zaidi,” aliongeza.
“Ni aibu kuwa wahudumu wa afya waliokuwa wakiandamana kwa amani, ambao kazi yao ni kulinda maisha ya wananchi, walikumbana na ukatili. Wanne walijeruhiwa. Tunataka IPOA ichukue hatua, na Inspekta Jenerali Douglas Kanja aombe msamaha hadharani. Tunataka kuonyeshwa hatua iliyochukuliwa dhidi ya polisi waliohusika.”
Odipo Nicholas, Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Wataalamu wa Maabara za Matibabu, pia alilaani ukatili wa polisi, akimtaka Inspekta Jenerali atoe ushahidi wowote wa uharibifu wa mali uliofanywa na waandamanaji wa UHC uliosababisha matumizi ya nguvu.
“Tungependa kujua kama maandamano yamepigwa marufuku nchini. Vuvuzela na filimbi wanazotumia waandamanaji wa UHC zimegeuka kuwa silaha?” alihoji.
Bw Odipo pia alishutumu Wizara ya Afya na serikali za kaunti kwa kuwakandamiza wafanyakazi 97 wa Global Fund ambao mikataba yao ilimalizika Juni 2024, lakini wameendelea kufanya kazi bila malipo kwa miezi 11 sasa.
Kulingana naye, mikataba yao ilijumuisha kipengele cha kuajiriwa kazi za kudumu baada ya mkataba kuisha. Wale walioajiriwa chini ya serikali kuu waliingizwa kwenye ajira za kudumu na sasa wanapokea mishahara bila kukatizwa.
“Tunahitaji Wizara ya Afya na Baraza la Magavana kuitisha kikao cha dharura na vyama husika ndani ya siku 14 kuunda mfumo wa kuwaajiri wafanyakazi wote wa UHC na Global Fund kuanzia Julai 1, 2025, kulipa malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wa Global Fund, na kulipa mafao ya muda waliotumikia chini ya mikataba,” alisema.
Siku tatu zilizopita, magavana walikataa mpango wa kaunti kuwalipa wafanyakazi wa UHC wakisema hawana fedha.
Waziri wa Afya, Aden Duale, alipohojiwa kuhusu suala hilo alisema alikutana na viongozi wa vyama vya afya na kulijadili, na kuwa ikiwa wafanyakazi wa UHC wanahitaji malipo yao, wanapaswa kwenda bungeni kuomba fedha zitolewe kwa Wizara ya Afya ili waweze kuhamishiwa kwa kaunti na kulipwa kama ilivyopangwa.