Jimbo ambalo utatozwa faini ya karibu Sh4 milioni ukipatikana na panga
MELBOURNE, Australia
SERIKALI moja ya jimbo nchini Australia inapania kupiga marufuku uuzaji wa mapanga baada ya kijana mmoja kujeruhiwa katika mapigano yaliyohusisha genge moja la wahalifu waliyoyatumia kama silaha.
Waziri Mkuu wa jimbo la Victoria Jacinta Allan Jumatatu, Mei 27, 2925 alitangaza kuwa marufuku hiyo itaanza kutekelezwa Jumatano baada mapigano yaliyohusisha matumizi ya mapanga katika Jumba la Kibiashara la Melbourne Jumapili alasiri.
Mwanamume mwenye umri wa miaka 20 alijeruhiwa vibaya katika makabiliano kati ya wapiganaji waliojihami kwa mapanga, taarifa ya polisi ilisema.
Kufikia Jumatatu, washukiwa wanne walikuwa wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka.
“Nitaanzisha sheria nyingi (inavyohitaji) kuhakikisha kuwa visu hivi vikubwa havipatikani barabarani tena,” Allan akawaambia wanahabari.
“Tutaanzisha marufuku ya uuzaji wa mapanga hapa Victoria na marufuku hii itaanza kutekelezwa Jumatano adhuhuri. Kwa kuzingatia mamlaka yanayohusiana na bidhaa zinazouzwa, jimbo la Victoria litazima kabisa uuzaji wa mapango katika eneo lolote jimboni humu,” Waziri Mkuu huyo mwanamke, akaongeza.
Victoria ndilo jimbo la kipekee nchini Australia linalopania kuweka marufu kama hiyo.
Upanga unaainishwa kama kisu chenye urefu unaozidi sentimita 80 (karibu inchi 8).
Visu vinavyotumika jikoni vimesazwa na marufuku hiyo japo vimetumika katika maeneo kadhaa duniani, ikiwemo Kenya, kusababisha maafa kutokana na mizozo ya kinyumbani.
Baada ya marufuku iliyotangazwa na Waziri Mkuu Bi Allan kuanza kutumika Jumatano wiki hii, watakaokiuka hitaji na kupatikana na upanga watozwa faini ya dola 30,700 (Sh3,991,000 za Kenya, kifungo cha miaka mwili gerezani au adhabu zote mbili.
Mnamo Septemba mwaka jana mataifa ya Uingereza na Wales yalipiga marufuku umiliki wa mapanga na aina fulani za visu.
Australia pia ni miongoni baadhi ya nchi za ulimwengu zenye sheria kali kuhusu matumizi ya bunduki.