Aliyebwagwa kwa udiwani asaka mteja wa nyeti zake anazouza Sh500,000
Na PETER MBURU
MWANAMUME aliyebwagwa kwenye kinyang’anyiro cha udiwani katika Kaunti ya Migori anayedai kuwa muflisi sasa ametangaza kuwa anataka kuuza nyeti zake kwa Sh500,000, kuepuka uhawinde.
Ian- Harriet Kowiti (pichani) kutoka eneobunge la Uriri, Kaunti ya Migori amesema kuwa amechoshwa na maisha ya uchochole na sasa ameamua kutafuta pesa kwa kuuza korodani moja!
Mwanamume huyo aidha amesema kuwa yuko tayari kuuza figo moja kwa Sh1.5 milioni kwa mteja wa humu nchini, ama mara tatu ya pesa hizo kwa mteja kutoka nje ya nchi.
“Ina haja gani kuwa na korodani mbili kati ya miguu yangu wakati hata nikiwa na moja bado naweza kufanya ‘kazi’ vyema?” Kowiti akasema.
“Nataka kuuza kwa kuwa nimekosa pesa na pia sihitaji korodani mbili ili kuishi. Najua kuna mtu mahali amekosa mtoto kwa ajili ya tatizo kama hili,” akasema.
Katika uchaguzi uliopita, Kowiti ambaye ana miaka 27 alijaribu kuwania kama MCA huru katika wadi moja, lakini akabwagwa.
Anasema kuwa anapanga kuuza sehemu hiyo ili kuboresha maisha yake, japo akisema kiini kikuu si kupata pesa.
Lakini baadhi ya wataalamu wa masuala ya afya hawakubaliani naye kuwa mtu anahitaji kutolewa korodani moja kwa kuwa kunao wanaozaliwa na moja pekee.
Aidha, nchini Kenya hakuna wataalamu wala mashine za kutekeleza upasuaji wa aina hiyo.