• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
Kaunti ya Niarobi yakaangwa kutumia Sh6 milioni kurusha fataki

Kaunti ya Niarobi yakaangwa kutumia Sh6 milioni kurusha fataki

Na COLLINS OMULO

SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi imekosolewa vikali kwa kutumia Sh6.3 milioni kufanya fataki wakati wa sherehe za Mwaka Mpya.

Matumizi hayo ni miongoni mwa maswali yanayoulizwa kwenye ripoti ya uchunguzi ya Mhasibu Mkuu wa Pesa za Serikali katika ripoti yake ya matumizi ya fedha ya mwaka wa kifedha ya 2016/2017.

Iliibuka kuwa Baraza la Jiji lilikiuka sheria kwa kutoa kandarasi kwa kampuni iliyotekeleza maonyesho hayo, bila ya kutangaza kwa umma ili waliotaka kutuma maombi wapate fursa ta kushiriki.

Aidha, mchunguzi huyo alikosoa utaratibu wa kulipa, ambapo hakukuwa na hati za kandarasi zilizoambatishwa vocha za malipo. Alisema ilikuwa vigumu kuthibitisha uhalali wa vocha hizo.

Alipofika mbele ya Kamati ya Bunge inayohusika na kufuatilia jinsi pesa za umma zinavyotumiwa katika Kaunti ya Nairobi, afisa wa mashirika na utalii, Machira Gichohi alitakiwa kuelezea alivyotoa kandarasi hiyo.

Mwakilishi wa Wadi ya Kilimani, Moses Ogeto alibainisha kuwa kabla ya utaratibu wa kutoa kandarasi hiyo, idara hiyo ilikuwa tayari imetoa vipimo vya fataki ambayo ingetumika kwa kampuni mbili.

Alisema kuwa kamati ya utoaji wa kandarasi ilifanya mkutano Desemba 22, 2016, siku kadhaa baada ya maagizo ya kandarasi (LPO) kutolewa kwa Tononoka Limited.

“Mkutano huo ulifanywa Desemba 22, 2016 ilhali LPO ilitolewa Desemba 18 na malipo yalifanywa Desemba 16. Hili linawezekana vipi?” aliuliza Bw Ogeto.

Bw Gichohi alipofika mbele ya kamati hiyo alishindwa kuelezea hitilafu hiyo lakini akatetea gharama iliyotumika katika ununuzi wa fataki na maonyesho kwa kusema sherehe kama hizo ni kivutio cha utalii jijini.

Sherehe hizo zilifanyika Desemba 31, 2016 usiku katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta (KICC) kukaribisha mwaka mpya.

Hii ni baada ya kamati hiyo chini ya usimamizi wa mwakilishi wa Mabatini kuzua maswali kuhusiana na kiwango cha fedha zilizotumiwa kwa kusema zilifaa kutumiwa katika miradi muhimu zaidi.

Mwakilishi maalum, Bi June Ndegwa alisema wakazi wa Nairobi wanahitaji maendeleo zaidi na utoaji bora wa huduma kuliko kuwavutia watalii kutokana na maonyesho ya fataki.

Lakini Bw Gichohi alipuuza kauli hiyo kwa kusema mwaka huu, maonyesho ya fataki yatakuwa makubwa zaidi.

You can share this post!

LSK yashtaki utekelezaji wa agizo la magari jijini

Huenda shule 50 zikafungwa kutokana na ukame

adminleo