Nyumba za wakazi 3,000 hatarini kusombwa na Bahari Hindi
Na Kalume Kazungu
WAKAZI zaidi ya 3000 wa miji ya Mkokoni na Kizingitini, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki wanaishi kwa hofu ya nyumba zao kufagiliwa na maji ya Bahari Hindi.
Hii ni kufuatia kuvunjika kwa kuta maalum zilizojengwa kandokando ya bahari maeneo hayo ili kuzuia maji yasivuke kuingia kwenye makazi ya binadamu.
Wakizungumza na Taifa Leo, wakazi walilalamikia hali mbaya ya kuta hizo ambazo wanadai kukosa kukarabatiwa kwa muda mrefu.
Katika kijiji cha Mkokoni, wakazi waliilalamikia serikali ya awali ya kaunti ya Lamu kwa kujenga kuta hizo kiholela, hatua ambayo imechangia kuharibika haraka kwa kuta hizo.
Bw Khaldun Vae ambaye ni mmoja wa wazee wa Lamu Mashariki, aliitaka Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) kuchunguza ubadhirifu uliotekelezwa na utawala wa awali wa Kaunti ya Lamu wakati wakijenga ukuta Mkokoni ambao haukudumu.
“Wananchi wetu kwa sasa wanahatarisha maisha yao kwa kuishi bila hizo ngome za kudhibiti nguvu za maji ya bahari yasifike majumbani mwao. Ujenzi wa ukuta wa Mkokoni ulifanywa miaka miwili iliyopita na tayari kuta zote zimeangushwa. Hii inamaanisha ujenzi ulikuwa wa ovyo na inastahili urudiliwe. EACC ifuatilie jambo hili. Kuna ubadhirifu wa fedha ulifanywa mahali,” akasema Bw Vae.
Katika kijiji cha Kizingitini, wakazi waliilalamikia serikali ya kitaifa kwa kukosa kukamilisha ujenzi wa ngome yao uliokuwa ukiendelezwa miaka minne iliyopita.
Wakazi kadhalika walisema baadhi ya kuta pia zimeangushwa kutokana na nguvu ya maji ya Bahari Hindi.
Bw Shee Kassim alisema sehemu zingine za ukuta pia zimebondekabondeka, hivyo kuruhusu maji kupita hadi karibu na makazi yao.
Waliitaka serikali ya kitaifa kuharakisha kukarabatiwa na kukamilishwa kwa ujenzi wa ngome hiyo ili wakazi waishi raha mstarehe.
“Kuta nyingi za bahari hapa Kizingitini zimezeeka na kuvunjika kutokana na nguvu ya maji ya bahari. Isitoshe, serikali yenyewe haikuwa imekamilisha mradi wa ujenzi wa kuta hizo. Ombi langu kwa serikali ni kusikia kilio chetu na kuzikarabati hizi ngome,” akasema Bw Kassim.