• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
BEATRICE OMOLLO: Muinjilisti wa Dandora anayelenga kuwa ‘Mama G’ wa Kenya

BEATRICE OMOLLO: Muinjilisti wa Dandora anayelenga kuwa ‘Mama G’ wa Kenya

Na JOHN KIMWERE

UKUAJI wa teknolojia duniani unaonekana unaendelea kuchochea wengi kujitosa katika ulingo wa tasnia ya filamu nchini. Hali inayobainisha wazi kuwa wapo wengi wenye talanta wanahitaji kupigwa jeki ili kuonekana na kutambuliwa.

Ndivyo ilivyo kwa mwigizaji wa kike, Beatrice Anyango Omollo (52) ambaye kando na umri wake ana malengo ya kufanya makubwa katika tasnia ya filamu.

Ndiyo mwanzo wa ngoma kwa mwigizaji huyu mjane, muinjilisti na mwanzilishi wa kanisa la ‘Jesus Explore Ministry (JEM)’ la mtaani Dandora, Nairobi.

”Ukweli ni kwamba ndani ya kipindi kirefu nimekuwa nikiwazia jinsi ningepata nafasi kuigiza kwenye kipindi cha ‘Mother In Law’ ambacho hurushwa hewani kupitia runinga ya Citizen TV,” alisema na kuongeza kuwa hali hiyo ilimchochea kuanzisha kikundi cha uigizaji kanisani kiitwacho ‘Waiting Upon The Lord’ miaka miwili iliyopita.

Kundi hilo limefaulu kufanya michezo sita ya kuigiza ikiwamo ‘Waiting Upon The Lord,’ ‘Mke Mwema,’ pia ‘Shujaa’, kulingana na maandiko ya Biblia takatifu.

Anasema katika mpango mzima wamepania kutumia uigzaji kuchochea jamii kwa jumla kubadili mienendo yao maana michezo yao inazingatia maandiko ya Biblia.

Anasema alianzisha kikundi cha uigizaji alipogundua kanisani mwake walikuwapo waumini wenye talanta ya uigizaji ila walikosa pa kuitumia. Kundi hilo linalenga kutengeneza muvi za injili ya Mungu na kupata sifa kama ilivyo filamu ya ‘Samson and Delilah’ ya Hollywood.

Kadhalika kando na kutengeneza muvi, kundi hilo lipo tayari kutembelea kanisa lolote duniani kuhubiri kupitia uigizaji. Hata hivyo anadai makundi mapya yanahitaji ufadhili ili kugharamia shughuli za kutekeleza jukumu hilo.

Kwa mara ya kwanza mchezo wao ‘Waiting upon the Lord’, ulifanikiwa kurushwa hewani kupitia runinga ya Mother and Child TV mwezi uliyopita.

”Ninataka kufika mbali katika tasnia ya filamu maana macho yangu yalenga kiwango cha staa wa Nollywood, mwigizaji, mwimbaji, mwana mitindo na dezaina shupavu nchini Nigeria Patience Ozokwor maarufu Mama G,’ alisema Beatrice.

Aliongeza msanii huyo humvutia kulingana na jinsi huonesha uhalisia wa mambo kwenye muvi zote ambazo ameshiriki.

Veterani huyo aliyewahi kufanya kazi kwenye redio stesheni tofauti nchini humo ameshiriki filamu kama ‘Blood Sister 2003,’ ‘2 Rats 2003,’ ‘The Wedding Party 2 2017,’ ‘Marcus D Milionaire,’ ‘Code of Silence 2015,’ ‘Abuja Top Ladies,’ ‘Turning Point 2012,’ na ‘The End is Near 2012,’ kati ya zingine.

Kwa wana maigizo mahiri duniani anapenda kuketi na kutazama kazi za waigizaji kama Leamy James pia Wagner Billyzane wa Marekani na Canada mtawalia.

Anasema akiwa mdogo alitunga nyimbo moja ya njili ya Mungu ila hakufaulu kuirekodi.

Beatrice anayejivunia kuwaona wajukuu watatu anataka Wakristo pia wajifunze zaidi neno ya Mungu kupitia kazi za uigizaji wake.

Anahimiza waigizaji wanaokuja kutovunjika moyo bali wajitume na kujitolea bila kulaza damu maana bidii yao ndiyo itafanikisha milango zaidi kufunguka.

You can share this post!

NLC kuwafidia wakazi wa Gatundu Kaskazini kwa ardhi ya...

Azimio langu ni kufikia upeo wa Mercy Johnson, asema Dorcas...

adminleo