Uhuru ashtakiwa kwa kuteua waliotemwa uchaguzini
Na Richard Munguti
MWANAHARAKATI Okiya Omtatah amewasilisha kesi kortini kupinga hatua ya Rais Uhuru Kenyatta na mawaziri kuwateua wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2017 katika nyadhifa kuu za mashirika ya umma na serikalini.
Mwanaharakati huyo anasema kuwa baadhi ya nyadhifa zilizojazwa na Rais Kenyatta hazipo katika katiba kama ule wa waziri msaidizi.
Bw Omtatah anasema Rais Kenyatta alikaidi sheria kwa kuwateua wanasiasa hao katika nyadhifa za wanachama na wakuu wa mashirika la Serikali.
Katika kesi aliyowasilisha jana Bw Omtatah amemshtaki Rais Kenyatta, Tume ya Kuajiri Watumishi wa Umma (PSC), Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi.
Bw Omtatah anasema uteuzi huo unakinzana na vipengee vya Katiba na anaomba Mahakama Kuu iufutilie mbali.
Mwanaharakati huyo anasema hakuna yeyote ameruhusiwa kutekeleza majukumu isipokuwa vile yametamkwa na kukubaliwa katika Katiba.
Alisema wadhifa wa waziri mwenye mamlaka makuu pia haupo katika Katiba.
Bw Omtatah amesema nyadhifa hizi zilipasa kutangazwa baada ya maoni ya wananchi kushirikishwa.
Alimlaumu Rais Kenyatta kwa kuwachagua watu kabla ya kuhojiwa.
“Ninaamini kuendelea kuingiliwa kwa katiba na sheria kunapasa kuchukuliwa kama jambo la dharura na kwapasa kusitishwa mara moja na Mahakama Kuu,” anasema Bw Omtatah.
Anaomba wadhifa wa waziri msaidizi ufutiliwe katika wizara zote.
Wanasiasa waliotemwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017 ni miongoni mwa watu ambao wameteuliwa na Rais Kenyatta na mawaziri wake kuhudumu katika nyadhifa kuu kwenye mashirika mbalimbali ya serikali.
Mbali na nyadhifa nyingi kukabidhiwa wanasiasa waliofeli kwenye uchaguzi uliopita, kigezo kingine kilichojitokeza ni vijana kuendelea kukaa kwenye baridi.
Teuzi hizo pia zinazua maswali kuhusu kujitolea kwa Rais Kenyatta na serikali yake katika kuheshimu Manifesto ya Jubilee.