2022: Ruto hapumui, pingamizi dhidi yake zapamba moto
Na SHABAN MAKOKHA na NDUNG’U GACHANE
JUHUDI za Naibu Rais William Ruto kutaka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi wa 2022 zinaendelea kupata pingamizi, huku viongozi wakimshinikiza kumtaka astaafu 2022.
Viongozi wa chama cha Ford Kenya ndio wa punde zaidi kusema hadharani kuwa msimamo wa aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe kuwa Dkt Ruto hapaswi kugombea urais 2022 ni sahihi.
Kinara wa Ford Kenya Moses Wetangula, Katibu Mkuu Dkt Eseli Simiyu na Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati, wanasisitiza kuwa mfumo wa utawala wa urais unajumuisha hata naibu wake, na lazima wote wastaafu pamoja hatamu yao itakapokamilika.
“Kulingana na Katiba, urais unakaliwa na watu wawili ambao ni Rais Kenyatta na Dkt Ruto. Muhula wa kuhudumu kwa Rais unapotamatika, naibu wake pia anafaa kustaafu naye,” akasema Dkt Simiyu.
Kifungu cha 148 (1) cha Katiba kinasema: “Kila anayetaka kuwania urais anamteua mtu aliyehitimu kuteuliwa kama rais, awanie kuwa Naibu wa Rais.” 148 (8) kinasema: “Mtu hatashikilia wadhifa wa Naibu Rais kwa zaidi ya mihula miwili.”
Wanasiasa wanaompinga Dkt Ruto wanatumia vifungu hivi vya Katiba kusisitiza kuwa anapaswa kustaafu pamoja na Rais kwa kuwa mbali na kuchaguliwa pamoja, wote hawaruhusiwi kushikilia nyadhifa zao kwa zaidi ya mihula miwili.
Hata hivyo, vifungu hivi havisemi lolote kuwa Naibu Rais hawezi kuwania urais
Mbunge huyo wa Kimilili alimtaka Dkt Ruto kuwaeleza Wakenya kile ambacho atawatekelezea akiwa rais, ambacho hajakifanya akiwa Naibu Rais.
“Ikiwa ndugu yetu Dkt Ruto ameongoza kwa pamoja na Rais Kenyatta kwa mihula miwili, kipi tena anakihitaji? Ni nini Dkt Ruto hajafanya anapokimbia huku na kule akizindua miradi ya maendeleo ambayo anasisitiza lazima ikamilike kufikia 2022?” akauliza Dkt Simiyu.
Wakizungumza katika eneo la Rosterman, Kaunti ya Kakamega wakati wa mazishi ya Rosebelea Simiyu, dadake Dkt Simiyu, viongozi hao kutoka Kaunti ya Bungoma waliitaka jamii ya Waluhya kuunga mkono azma ya urais ya Bw Wetangula hapo 2022.
Katika eneo la Mlima Kenya, kundi linalojumuisha wanasiasa walioshindwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 limezinduliwa kwa lengo la kuwakabili wale ambao wanaonekana kuegemea upande wa Dkt Ruto.
Kundi linaloongozwa na Mbunge wa Kuteuliwa, Maina Kamanda, linasema lazima lihakikishe wabunge hao wa kundi la ‘Tanga Tanga’ wanakabiliwa vilivyo kwa kuungana na Dkt Ruto katika siasa za 2022.
Baadhi ya viongozi wengine kwenye kundi la Bw Kamanda ni Bw Peter Kenneth, Bi Martha Karua na aliyekuwa mbunge wa Dagoreti, Bw Dennis Waweru.
“Sasa tuko na kikundi ambacho rais anaweza kukitegemea. Tutazunguka kote nchini kuwakumbusha wananchi kuwa muda wa rais kuongoza haujaisha,” akasema Bw Kamanda akiwa Murang’a.
Kauli ya kumtaka Dkt Ruto ang’atuke pamoja na Rais Kenyatta pia imewahi kutolewa na Naibu Kinara wa ODM, Bw Ali Hassan Joho na wabunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) na Muturi Kigano (Kangema).
Wiki jana, kinara wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka pia alinukuliwa akisema kuwa haoni ubaya wowote Rais Kenyatta akitafuta nafasi ya uongozi mwaka 2022.
Gavana wa Machakos, Alfred Mutua pia amewahi kunukuliwa akisema kuwa Dkt Ruto ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe wanaopaswa kustaafu, kwa kuwa muda wao wa kuongoza utakamilika 2022. Hii ni licha ya kuwa Dkt Ruto ana umri wa miaka 52 na hivyo kauli kuhusu ukongwe wake haina mashiko.