Habari za Kitaifa

Wakili na mwanablogu aliyetoweka Ndiang’ui Kinyagia ajitokeza, ajiwasilisha kortini

Na BENSON MATHEKA July 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKILI na mwanaharakati wa mtandao, Bw Ndiang’ui Kinyagia yuko hai na salama, siku kadhaa baada ya kuripotiwa kutoweka katika hali ya kutatanisha.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na wakili wa familia yake, Bw Wahome Thuku Alhamisi Julai 3, 2025, Bw Kinyagia aliwasiliana na jamaa yake Jumanne jioni na kuthibitisha kuwa yuko salama.

Kinyagia, ambaye ni mwanablogu, alitoweka wiki iliyopita, hali iliyoibua taharuki na shinikizo hasa kupitia mitandao ya kijamii serikali ikilaumiwa kwa dai alitekwa na maafisa wa usalama waliozingira na kuvunja nyumba yake.

Wakili Wahome  alisema kuwa Bw Kinyagia alieleza jamaa zake kwamba alijificha kwa muda baada ya kupata habari kuwa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walikuwa wakimtafuta kwa madai ambayo hajaelewa hadi sasa.

“Ndiangui alisema alihofia maisha yake  na akaamua kujificha hadi pale ambapo angehakikishiwa usalama wake,” alisema Thuku

Kwa mujibu wa wakili huyo, Bw Kinyagia yuko tayari kujisalimisha kwa maafisa wa DCI na kufikishwa mahakamani, lakini tu ikiwa usalama wake utahakikishwa. “Tumemshauri ajitokeze rasmi leo, Alhamisi, Julai 3, saa tano asubuhi katika Mahakama ya Milimani,” alisema.

Wakili Thuku alisema kuwa habari za kupatikana kwa Bw Kinyagia tayari zimewasilishwa kwa Chama cha Wanasheria Kenya (LSK).

Mahakama ilikuwa imeamuru kuwa DCI na Inspekta Jenerali wa Polisi wamwachilie Kinyagia au wamfikishe mahakamani.

“Kupotea kwa Kinyagia kulizua hofu kubwa kwa familia na umma. Tumefarijika kuwa yuko salama, na sasa tunalenga kuona haki inatendeka,” alisema Thuku.

Familia ya Ndiangui ilidai kuwa maafisa wa DCI walivamia nyumba yake huko Kinoo Juni 21, wakivunja mlango bila kibali cha mahakama na kuchukua vifaa kadhaa, zikiwemo kompyuta, simu, pasipoti na kadi ya chanjo ya homa ya manjano. Wakati huo Bw Kinyagia hakuwa nyumbani.

Tukio hilo lilipelekea familia kuripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Kinoo,

DCI ilikana kumzuilia Kinyagia na kusema kuwa alikuwa anatafutwa kwa uchunguzi wa chapisho mtandaoni, hasa kuhusu maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z yaliyofanyika Juni 25.