Raila afokea Ruto kwa kuamuru waandamanaji wapigwe risasi
Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, amekosoa vikali agizo la Rais William Ruto kwa maafisa wa polisi kuwapiga risasi waandamanaji miguuni ghasia zikizuka wakati wa maandamano, akionya kuwa agizo hilo linahalalisha matumizi ya nguvu kupita kiasi na ni dharau kwa utawala wa sheria.
Kupitia taarifa jana, Raila, ambaye ni mshirika wa Ruto katika serikali Jumuishi alisema kuwa agizo lolote kwa polisi kuwapiga risasi kwa lengo la kuua, kulemaza, kuwatatiza au kuwatisha raia si sahihi na ni kinyume na misingi ya utawala wa sheria.
“Katika maandamano au mazingira yoyote yanayohitaji utekelezaji wa sheria, maagizo haya ya kupiga risasi kwa lengo la kuua, kulemaza au kuwatatiza raia si sahihi,” alisema Raila.
Waziri mkuu huyo wa zamani, alisisitiza umuhimu wa kufuata utawala wa sheria na kuepuka matumizi ya nguvu kupita kiasi na matumizi mabaya ya mamlaka dhidi ya raia.
“Kama taifa, lazima kila wakati tuchague kufuata utawala wa sheria na taratibu zinazofaa, na tukatae vishawishi vya kuwapa polisi mamlaka haramu ya kutumia nguvu dhidi ya raia, hata ikiwa raia hao wanashukiwa kuvunja sheria,” aliongeza.
Kauli yake imejiri wakati ambapo kumekuwa na lawama kali za kitaifa na kimataifa kuhusu mwenendo wa polisi katika maandamano ya kupinga serikali yaliyofanyika hivi karibuni.
Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR), inayofadhiliwa na serikali, imeripoti kuwa watu 31 wameuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika maandamano ya Saba Saba yaliyofanyika Julai 7, huku zaidi ya watu 500 wakikamatwa.
“Mtu yeyote anayepatikana akichoma biashara au mali ya mtu mwingine apigwe risasi mguuni, alazwe hospitalini, na kisha apelekwe mahakamani. Msimuue, lakini hakikisheni miguu yao imevunjika,” alisema Ruto jijini Nairobi siku ya Jumatano.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu ya kimataifa yameshtumu Kenya kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi na risasi dhidi ya waandamanaji wasio na silaha.
Ruto, aliyekuwa na hasira, aliwalaumu watu wasiojulikana kwa kufadhili wahuni, vurugu, na maandamano ya hivi majuzi nchini, akisema serikali haitakubali juhudi za kuvuruga utulivu wa nchi.
“Nimevumilia sana watu wanaotaka kubadilisha serikali kwa njia zisizo za kikatiba. Lakini sasa imetosha,” alisema Rais.
Raila alikosoa vikali kauli hiyo ya Ruto na kuitaka serikali kukabiliana na waandamanaji wanaozua fujo kwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani badala ya kutumia risasi, akisema hiyo ndiyo njia ya kulinda utu na haki za binadamu za washukiwa.
“Tunafanya vyema kama taifa tunapozingatia kuwa kila mtu hana hatia hadi anapopatikana na hatia na mahakama halali na yenye mamlaka ya kufanya hivyo,” aliongeza Raila.
Alikosoa mwelekeo wa kutumia nguvu na ukatili katika usimamizi wa usalama, akitaka agizo hilo la Ruto liondolewe kabisa. “Kama taifa, tunapaswa kufanya kila juhudi kuepuka kugeuza polisi kuwa jeshi la vita,” alisema Raila.
Aliongeza kuwa mifano kutoka nchi nyingine za Afrika inaonyesha kuwa njia hiyo huongeza tu hatari ya vurugu zaidi.Kauli ya Rais Ruto ilijiri wakati ambapo mvutano unazidi kupamba moto huku maandamano ya vijana dhidi ya sera za serikali yakiendelea kuenea kote nchini, wakitaka uwajibikaji na mageuzi.
Matamshi ya Rais yamezua mjadala, hasa katika muktadha wa heshima na ulinzi wa haki za binadamu, ambazo zimekuwa zikikiukwa katika miezi ya hivi karibuni polisi wakihusishwa na utekaji nyara na mauaji wakati wa maandamano ya amani.