• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
ANC yalia kudhalilishwa na ODM

ANC yalia kudhalilishwa na ODM

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Amani National Congress (ANC) kimelalamikia kuondolewa kwa Mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba kutoka kwa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC), kikisema hakishauria kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa.

Naibu kiongozi wa chama hicho Ayub Savula amesema kuwa japo nafasi hiyo ilipewa mbunge maalum wa chama hicho Godfrey Osotsi, kiranja wa wachache Junet Mohammed aliyefanya mabadiliko hayo alipaswa kushauriana na uongozi wa chama hicho.

“Hii sio ungwana hata kidogo. Ni makosa kwa ODM kuondoa mwanachama wetu katika kamati ya HBC bila kutufahamisha. Ingawa aliyechukua nafasi huyo ni mwanachama wetu, tulipasa kushauriwa kwanza kabla ya mabadiliko hayo kutekelezwa,” Bw Savula, ambaye ni mbunge wa Lugari akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

“Leo (Jumanne) nilifika bunge na kushangaa kuona jina la Mheshimwa Osotsi miongoni mwa wale waliopendekezwa kuwa wanachama wa HBC. Nilipomuuliza kiongozi wa chama chetu, Bw Musalia Mudavadi ikiwa ana habari kuhusu mabadiliko hayo, alisema hana habario zozote,” akaongeza mbunge ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kundi la wabunge wa ANC.

Bw Savula alisema Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) ya ANC itaiandikia barua ODM ikilalamikia kuondolewa kwa wanachama wake kutoka kamati za bunge pasina kushauriwa, kitendo ambacho alisema ni kielelezo dharau dhidi ya chama hicho.

“Kama familia ya NASA, tunafaa kuheshimiana. Lakini huu mwenendo wa ODM kudharua vyama tanzu katika muungano huo unaenda kinyume cha falsafa iliyobuni muungano huo,” akasema.

Katika orodha hiyo iliyoidhinishwa jana bungeni, kando na Bw Osostsi wawakilishi wengine wa NASA ni; Mishi Mboko (Likoni, ODM) na Dkt Makali Mulu (Kitui ya Kati, Wiper). Na upande wa Jubilee kuna wabunge; Amos Kimunya (Kipipiri), Shadrack Mose (Kitutu Masaba), Bi Kawira Mwangaza (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Meru) na Joyce Emanikor (Mbunge Mwakilishi wa Turkana).

Jaribio la Bw Milemba kujaribu kalalamikia kutemwa kwake kulizimwa na Spika Justin Muturi aliyeshikilia kuwa orodha hiyo haitafanyiwa mabadiliko yoyote.

“Bw Milemba, tulia… tulia… hapa ni bunge chumba ambacho kina taratibu zake. Huu sio mkutano wa Kuppet ambao wewe ni kiongozi. Ikiwa una malalamishi yoyote, utayawasilisha kesho lakini sio leo (Jumanne),” akasema.

Akitetea uteuzi wa Bw Ososti kiongozi wa wachache John Mbadi alisema mrengo huo uliamua kufanya mabadiliko hayo ili kutoa nafasi kwa “wanachama wetu wengine kupata uzoefu kuhusu namna ratiba ya shughuli za bunge huandaliwa.”

You can share this post!

Pacha waungama kushiriki ngono na mpenzi mmoja

Polisi washindwa kueleza jinsi matamshi ya Kuria yangezua...

adminleo