Habari za Kitaifa

UDA ya Ruto na ODM ya Raila zakabana kuhusu Sh30 milioni ada za mawakili

Na JOSEPH WANGUI July 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kimepata afueni katika mvutano wake na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) pamoja na vyama vingine vitano vya kisiasa kuhusu malipo ya Sh30 milioni kama ada za mawakili.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu kusitisha zoezi la kukadiria ada hiyo hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa uamuzi kuhusu rufaa iliyowasilishwa na UDA kupinga agizo la kubebeshwa gharama hizo.

Mzozo huu unatokana na gharama za kesi mwaka 2023 kuhusu usambazaji wa Hazina ya Vyama vya Kisiasa, ambapo UDA ilidai kutotendewa haki katika mgao wa fedha.

Gharama hizo zilitokana na uamuzi wa Mahakama Kuu mnamo Mei 11, 2023, ambapo madai ya UDA kuwa sehemu ya mgao wake wa fedha ulipelekwa kwa vyama kama ODM, Jubilee, Maendeleo Democratic Party, Chama cha Uzalendo, Progressive Party of Kenya, na Devolution Empowerment Party, yalikataliwa na mahakama ikatoa agizo UDA kubeba gharama.

Hata hivyo, juhudi za ODM za kuanza mchakato wa kukadiria ada ya mawakili zilipata pigo baada ya Mahakama Kuu kusitisha zoezi hilo kufuatia ombi la UDA.

Jaji Anthony Mrima alisitisha mchakato huo hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa uamuzi katika rufaa ya UDA dhidi ya uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu.

Rufaa hiyo pia inahusu madai ya UDA kwamba ilinyimwa mgao wa ziada wa Sh115 milioni, kando na Sh577 milioni ilizopewa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa kwa mwaka wa kifedha ulioishia Juni 2023.

Katika ombi lake la kuzuia ukadiriaji wa ada, chama cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto, kilisema utekelezaji wa hukumu hiyo kwa njia ya ukadiriaji wa ada ungedhoofisha mchakato wa rufaa.

UDA ilieleza kuwa maagizo ya kuzuia zoezi hilo yalikuwa muhimu kwani ODM ilikuwa tayari imeanzisha mchakato wa kukadiria gharama, jambo ambalo lingeondoa maana ya rufaa iliyowasilishwa.

Chama hicho kilisema kuwa ukadiriaji huo ulikuwa wa mapema mno kwani inapaswa kusubiri uamuzi wa rufaa.Kwa upande wake, ODM ilipinga ombi hilo, ikitaka UDA ilazimishwe kuweka Sh15 milioni ambazo ni nusu ya gharama hiyo katika akaunti ya pamoja ya benki inayozalisha riba, itakayodhibitiwa na mawakili wa pande zote mbili, kama sharti la kusitisha utekelezaji wa malipo.

Chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga kiliambia jaji kuwa kwa kuwa ada hizo hazijakadiriwa bado, hakuna tishio la haraka la kutekelezwa kwa hukumu hiyo.

ODM ilisema ni kwa manufaa ya haki mchakato wa ukadiriaji uendelee bila kusumbuliwa kwani haijulikani rufaa hiyo itakamilika lini.Wakili wao aliongeza kuwa hata kama rufaa itafaulu baada ya utekelezaji wa hukumu, gharama hizo zinaweza kurejeshwa.

Hata hivyo, Jaji Mrima alisema kusitisha zoezi hilo kutasaidia kuharakisha uamuzi wa mzozo huo.Aliongeza kuwa baada ya rufaa kuamuliwa, ukadiriaji utaendelea kutoka pale ulipofikia, kulingana na maagizo au mwelekeo wowote wa Mahakama ya Rufaa.

“Ni jukumu la mahakama hii kuchukua msimamo unaohakikisha matumizi bora ya muda wa mahakama ambao tayari ni mdogo,” alisema Jaji Mrima.

Katika kesi ya awali, iliyotupiliwa mbali na Jaji Aleem Visram, UDA ilidai kuwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa alikosea katika kuhesabu jumla ya kura zilizopigwa kwa vyama vinavyofaa kupata ufadhili katika uchaguzi wa Rais.

Wabunge, Magavana na Madiwani.UDA ilidai kuwa msajili aligawa fedha kwa njia isiyo ya haki, akikiuka Sheria ya Vyama vya Kisiasa, hivyo kuvipa vyama vingine faida isiyo ya haki.

OKesi hiyo ilianzia katika Jopo la Kutatua Migogoro ya Vyama vya Kisiasa, ambayo pia ilitupilia mbali madai ya UDA.UDA ilikerwa kuwa msajili hakujumuisha kura kutoka kwa Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kericho na MCA wa Wadi ya Ravine, Kaunti ya Baringo, ambao walitangazwa washindi bila kupingwa.Lakini Jaji Visram alitupilia mbali dai hilo akisema hoja ya UDA haikuwa na mashiko ya kisheria.