Umaarufu wa China waongezeka Kenya wa Amerika ukipungua
China imeendelea kujizolea umaarufu miongoni mwa Wakenya kama mshirika wa kiuchumi, ikipunguza ushawishi wa Amerika, kulingana na utafiti mpya wa Pew Research Center.
Utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 48 ya Wakenya wanapendelea serikali kushirikiana zaidi na China kiuchumi ongezeko kutoka asilimia 38 mwaka 2019. Hii inaifanya China kufikia kiwango sawa na Amerika, ambayo imeshuka kutoka asilimia 52 hadi 48 katika kipindi hicho.
Tangu kuzinduliwa kwa mpango wa Belt and Road Initiative (BRI), China imewekeza sana nchini Kenya kupitia mikopo ya kufadhili miradi ya miundombinu kama reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Suswa, barabara ya Nairobi Expressway, Thika Road, na barabara za kuzunguka jiji la Nairobi.
China sasa ndiye mkopeshaji mkubwa wa Kenya, ikiwa na deni la zaidi ya Sh651 bilioni kufikia Machi 2025. Zaidi ya hayo, asilimia 71 ya Wakenya wanaona uwekezaji wa China kama mzuri kwa sababu huleta ajira , ikiongoza miongoni mwa nchi 24 zilizofanyiwa utafiti.
Biashara kati ya Kenya na China imeendelea kukua, huku bidhaa za thamani ya Sh576 bilioni zikiagizwa kutoka China mwaka jana. Hata hivyo, mizani ya biashara imeegemea upande wa China, kwani Kenya iliuza bidhaa za thamani ya Sh26 bilioni pekee.
Kwa upande wa Amerika, biashara haijaegemea sana: Kenya ilinunua bidhaa za Sh155 bilioni na kuuza bidhaa za Sh88 bilioni mwaka 2024. Hata hivyo, mazungumzo ya makubaliano mapya ya biashara kati ya Kenya na Amerika yamekwama tangu kubadilika kwa tawala katika mataifa yote.
Ushirikiano wa Kenya na Amerika kwa miaka mingi umekuwa zaidi katika masuala ya usalama, kudumisha na amani, na vita dhidi ya ugaidi. Hata hivyo, ziara ya Rais William Ruto nchini China mwezi Aprili ilizua maswali miongoni mwa baadhi ya wanasiasa wa Amerika kuhusu uhusiano wa karibu wa Kenya na China.
Seneta Jim Risch wa Idaho alisema, “Ruto ametangaza kuwa Kenya na China ni wabunifu na washirika wenza wa mpangilio mpya wa dunia. Huu si ushirikiano tu, bali ni utiifu wa Kenya kwa China.” Aliongeza kuwa ni wakati wa Amerika kufikiria upya uhusiano wake na mataifa kama Kenya.
Utawala wa Rais wa zamani Donald Trump ndio ulianzisha mazungumzo ya makubaliano ya biashara huru (FTA) na Kenya Februari 2020. Hata hivyo, utawala wa Rais Joe Biden ulisitisha mpango huo, ukapendekeza mpango mdogo wa US-Kenya Strategic Trade and Investment Partnership (STIP) ambao bado haujakamilishwa.
Mwakilishi wa biashara wa Amerika, Jamieson Greer, ambaye ni mshauri mkuu wa Rais Trump kuhusu masuala ya biashara, alisema mwezi Aprili baada ya kukutana na mwenzake wa Kenya, Bw Lee Kinyanjui, kwamba Amerika bado inataka kuendeleza mazungumzo hayo ya kibiashara.