Habari Mseto

Ndege iliyoua watu 5 Kericho ilikuwa na hitilafu ya injini – Wataalamu

February 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

 RICHARD MAOSI NA ERIC MATARA

HITILAFU katika injini ya ndege huenda ndicho kiini cha ajali iliyosababisha vifo vya watu watano, wanne kati yao wakiwa raia wa Marekani na Mkenya mmoja Jumatano.

Uchunguzi wa kina kutoka kitengo cha wataalamu wa ndege Aircraft Accident Investigations Division (AAID), wakishirikiana na polisi walibaini ndege ilipoteza mwelekeo kabla ya kugonga mti na kuanguka katika shamba la mtu binafsi eneo la Kamwingi karibu na msitu wa Londiani, Kaunti ya Kericho.

“Ni dhahiri kulikuwa na matatizo katika injini lakini tumechukua mabaki ya ndege na wale walioaga ili kufanya uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali,” afisa wa AAID alisema.

Aidha polisi walichukua rununu za waliopoteza maisha katika mkasa wa ajali.

Mali yao ililitapakaa kila sehemu, polisi wakilazimika kuzungusha uzio ili kudhibiti umati wa watu waliofika katika eneo la tukio.

Ndege nzima hasa sehemu ya mbele ilikuwa imevunjika ishara tosha kuwa walioabiri walipata maumivu mabaya.

Sehemu za ndege zikiwa zimeachana na kurundika kila mahali bila mpangilio.Viti vilikuwa vimevunjika na kuinamiana huku mikanda ya usalama ikiwa imekatika.

Ajali yenyewe ilitokea baada ya ndege aina ya Cesna 206-5-Y kupoteza dira angani na kuanguka ghafla ndani ya shamba la mkazi wa Kamwingi, kilomita tisa kutoka mjini Londiani.

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni mkenya mmoja,na raia wanne wa kigeni ambao inaaminika ni wa familia moja.

Polisi walisema ndege ilikuwa imesajiliwa kwa jina la David Mutava Mulwa lakini haikubainika moja kwa moja endapo ndiye alikuwa rubani wakati wa ajali.

Majina ya raia wa kigeni waliotambuliwa kutokana na stakabadhi zilizopatikana ni pamoja na Richard Carl Sednaoui 32 na Melissa Witt 28 wote raia wa Marekani.

Wanaume watatu na wanawake wawili wakipoteza maisha yao katika mkasa huo.

Kamishana wa kaunti ya Kericho James Mugera alidhibitisha kuwa ni watu watano waliopoteza maisha yao katika ajali.

“Miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Kericho kufanyiwa uchunguzi kabla ya kutambuliwa na familia zao,”Mugera alisema.

Ndege yenyewe ilikuwa ikiwasafirisha watalii kutoka eneo la Ol Kiombo Maasai Mara,kuelekea Lodwar kaunti ya Turkana.

Kwa mujibu wa walioshuhudia,ndege ilianza kuyumba karibu saa tano asubuhi.

“Ndege ilianza kuyumba kabla ya kuzima ingali angani,baadaye tulisikia mshindo mkubwa baada ya kuangukia mti ,” Timothy Koech alisema.

Mkazi mwingine aliyefahamika kama James Tanui alisema wakazi wengi walifika katika sehemu ya tukio wakitarajia kuokoa maisha ya walipoteza maisha papo hapo.

“Tulikuta tayari wamepoteza maisha na hatukua na jingine la kufanya,” alisema Tanui mwenyeji aliyekuwa miongoni mwa waliotangulia kufika katika eneo la tukio.

Mamia ya wakazi walitazama tukio kwa woga huku,polisi,wakisafirisha miili kwenye gari la Msalaba Mwekundu.

Miili ilihifadhiwa ndani ya mifuko na kupelekwa ndani ya magari ya shirika la msalaba mwekundu.

Ajali nyinginezo ambazo zimewahi kutokea katika kaunti ya Nakuru na kutikisa dunia ni mkasa ambao ndege ilitumbukia ndani ya ziwa Nakuru Octoba 21,mwaka wa 2017.

Ndani yake walikuwa wasafiri watano waliopoteza maisha yao na ilichukuwa muda wa wiki mbili kutafuta maiti zao.

Shughuli ya uokozi ilifanikiwa kupata miili mitatu kati ya watu tano walioangamia katika mkasa huo.

Walioangamia katika ajali hiyo alikuwa ni rubani Apolo Malowa,Antony Kipyegon.Sam Gitau,John Mapozi na Veronica Muthoni katika kampeni ya kufanikisha Susan Kihika kuwa seneta wa kaunti ya Nakuru.

Mwili wa Mapozi na Veronica Muthoni haijawahi kupatikana mpaka sasa.

Mnamo Juni mwaka uliopita ndege aina ya Flysax ilianguka ndani ya msitu wa Abedares na kuua jumla ya watu kumi.

Ndege hiyo iliyosajiliwa chini ya 5Y-CAC ilitoka Kitale kuelekea Nairobi,siku ya Jumanne tarehe 5 saa 4.05 jioni lakini ilikata mawasiliano mwendo wa saa 5.20 jioni,kabla ya kupotea lakini ilipatikana baada ya siku tatu.

Mwaka wa 2006 watu 14 walipoteza maisha yao miongoni mwao wakiwa ni wabunge tano katika eneo la Marsabit.Ajali ilitokea ndege ilipojaribu kutua baada ya hali ya anga kuwa mbaya.

Miongoni mwa viongozi waliopoteza maisha alikuwa ni Bonaya Godana, Mirugi Kariuki, Titus Ngoyoni, Abdi Sasura na Guracha Galgallo.

Miaka sita iliyopita 2012 Profesa George Saitoti na Orwa Ojode walipoteza maisha yao katika milima ya Ngong katika ajali mbaya kuwahi kushuhudiwa. Aidha walinzi wawili Thomas Murimi na Joshua Tongei hawakunusurika .Pamoja na marubani Nancy Gituanja na Luke Oyugi walioaga.

Siku hiyo ndege ilikua ikielekea katika eneo bunge la Ndiwa katika mkutano wa kuchangisha pesa.

Ajali kubwa ya ndege iliyowahi kufanyika katika nchi ya Kenya ni ile ya 1992 ambapo watu 46 walipoteza maisha yao wakiwa ndani ya ndege la kijeshi katika eneo la Kaloleni.Maafisa wengine sita walipoteza maisha yao wakiwa ardhini.

Januari 2000 ndege ya KQ431 kutoka Abijan Lagos kuelekea Nairobi ilianguka ndani ya Bahari ya Atlantic ikiua watu 169 lakini watu kumi walinusurika kifo na kuponea.Ajali hiyo ilitokea saa chache baada ya kutoka katika uwanja wa ndege wa Ivory Coast.

Mnamo 2007 KQ507 kutoka Abijan ilisimama Duala kabla ya kuelekea Nairobi lakini ikaanguka katika chemichemi ya maji, watu wote 114 walioabiri wakipoteza maisha yao.