Jinsi ODM inavyojiunda upya kwa uchaguzi wa 2027
CHAMA cha ODM kimeanzisha mpango wa kujipa sura mpya, kikiimarisha asasi zake ili kijivumishe mashinani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Wiki jana, Kamati Kuu ya chama hicho iliratibu shughuli kadhaa za kuadhimisha miaka 20 tangu kuundwa kwake huku kilele kikiwa Kongamano ya Kitaifa la Wajumbe (NDC) litakalofanyika Oktoba mwaka huu.
Maadhimisho hayo almaarufu, “ODM@20” yatafanyika katika kaunti zote 47 ambako viongozi wa chama wanatarajiwa kuelezea historia ya ODM na mafanikio yake huku wakitoa mwelekeo mpya unaofungamana na mabadiliko katika ulingo wa siasa wakati huu.
Jana, Ijumaa kiongozi wa ODM Raila Odinga aliongoza mkutano wa kwanza wa wajumbe wa chama hicho mjini Kakamega, kama sehemu ya shughuli za maadhimisho hayo.
“Hizi sherehe zitafanyika katika kaunti zote, kabla ya kongamano kubwa la kitaifa Oktoba mwaka huu. Safari ya ODM ya miaka 20, mafanikio yake na mustakabali wake utajadiliwa katika kongamano hilo,” Bw Odinga akasema.
Naye Katibu Mkuu ODM Edwin Sifuna alisema NDC itachambua ripoti kutoka kwa asasi za chama, kuangalia upya sera za chama na kutoa mwelekeo wa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Bw Odinga anasema maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa ODM sio sherehe tu “bali wakati wa chama chetu kujifufua na kujipa sura mpya.
“Tumetimu miaka 20 na tumeanza hapa leo (jana) na tutazunguka kote Kenya tukikutana na wajumbe wetu kabla ya kuchagua maafisa wapya katika NDC na kusherehekea safari yetu,” Bw Odinga akawaambia wajumbe mjini Kakamega.
Kiongozi huyo wa ODM alieleza kuwa chaguzi za mashinani zilizoanza Aprili mwaka huu na kuendelea hadi Agosti ni sehemu ya juhudi za kukijenga upya chama hicho.
Juhudi hizo pia zinaonekana kama zinazolenga kuisaidia ODM kukabiliana na changamoto zilizoikumba tangu ipoteze uchaguzi wa urais 2022 na kushuka kwa umaarufu kwa kushirikiana na chama cha UDA, chake Rais William Ruto.
Duru katika ODM zinasema kuwa chama hicho sasa kinalenga kuachana na siasa za makabiliano na kukumbatia siasa zinazoongozwa na sera na maono.
Wachanganuzi wa maswala ya siasa wanasema japo historia ya kisiasa ya ODM inajulikana, kuanzia enzi za Pentagon, Handisheki na BBI, changamoto yake kuu inasalia uwiano na uongozi bora.
“Huu ndio wakati wa ukweli kwa ODM,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismas Mokua.
“Shughuli ya kujipa sura mpya itafaulu tu ikiwa itazalisha uongozi halali na thabiti, sio wale wa kawaida wanaotunukiwa kwa misingi ya uaminifu,” akaeleza.
Kwenye mahojiano na runinga ya NTV wiki jana, Bw Odinga alisema ODM inayo hazina kubwa ya viongozi wenye umri mdogo wanaoweza kutwaa nafasi za uongozi.
Alidai kuwa ametumia miaka mingi akiwakuza viongozi wachanga kuanzia Bungeni hadi ngazi za mashinani, baadhi yao sasa wakiibuka kuwa na ushawishi katika ngazi ya kitaifa.
“Ndio nimezingirwa na viongozi wengi wachanga katika ODM,” Raila akasema.
“Unaweza kuwaona, ni wengi zaidi,” akaeleza.
Bw Odinga alitoa orodha ya viongozi kadhaa wa ODM, miongoni mwao akiwa Sifuna, Waziri wa Fedha John Mbadi, Waziri Uchumi wa Majini Hassan Joho, Mwenyekiti wa ODM Glady Wanga na Gavana wa Mombasa Abdulswamada Sheriff Nassir.
“Niko na watu kama Sifuna, Mbadi, Joho, Oparanya, Wanga na Nassir. Pia niko na viogozi vijana katika Bunge pamoja na madiwani kote nchini,” akasema .