Habari MsetoSiasa

BBI yapinga kuingiliwa kisiasa

February 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

KAMATI iliyoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuzunguka nchini ikikusanya maoni ya wananchi kuhusu masuala ya uongozi, Building Bridges Initiative (BBI) imepinga  kuiingiliwa kisiasa katika utendakazi wake, ikisema tangu ilipoanza kazi, hali imekuwa shwari.

Timu hiyo, hata hivyo, imesema kuwa huenda isiweze kukamilisha kazi yake kwa muda uliopangwa, ikisema hadi sasa imezuru kaunti 15 pekee nchini, kujadiliana na wananchi.

Ilitaja suala la kucheleweshwa kwa bajeti iliyotengewa na serikali mwaka uliopita kuwa lililoipelekea kuchelewa kuanza kazi, sasa ikisema inahitaji angalau miezi sita kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti kwa Wakenya.

Wanachama wa jopokazi la Building Bridges Initiative katika kikao na washikadau jumba la KICC mnamo Februari 14, 2019. Picha/ Peter Mburu

Jumatano, jopokazi hilo liliandaa vikao na washikadau kutoka sekta tofauti katika Jumba la makongamano ya kimataifa (KICC), ambao waliwasilisha mapendekezo yao, kuchangia ripoti itakayoundwa.

Timu hiyo ilikutana na Profesa Karuti Kanyinga, Taasisi ya Wakaguzi Hesabu za Pesa Nchini (ICPAK), Muungano wa Madaktari (KMPDU) na Muungano wa Waajiri (FKE)

Naibu Mwenyekiti wa jopokazi hilo Dkt Adams Oloo alisisitiza kuwa katika kaunti 15 ambazo jopokazi hiyo imezuru nchini hadi sasa, imepokea maoni ya washikadau bila matatizo, wala kuingiliwa na wanasiasa.

“Tumezuru kaunti 15 na hivyo bado tuna kazi nyingi ya kufanya. Tumejadiliana na washikadau tofauti na hakuna changamoto ya wanasiasa imeweza kututatiza. Kazi yetu ni kusikiza wananchi na viongozi, mambo ya siasa hayajaingilia shughuli za jopokazi,” akasema Dkt Oloo.

Profesa Karuti Kanyinga alipofika mbele ya jopokazi la BBI kuwasilisha mapendekezo yake mnamo Februari 14, 2019. Picha/ Peter Mburu

Akiwasilisha ripoti ya ukaguzi baada ya kufanya utafiti kaunti zote nchini, Prof Kanyinga alikosoa hali ya baadhi ya afisi za umma kukosa maelekezo mahususi kuhusu kazi yake na kuwepo kwa hali ya afisi kadha kuwa na mkanyagano wa utendakazi kuwa baadhi ya changamoto zinazokumba taifa na kufanya mzigo wa mishahara kupanda kupindukia.

Prof Kanyinga alifanya utafiti kwa ushirikiano na Shirika la Kukusanya na Kuhifadhi Takwimu Nchini (KNBS), ambapo walihoji familia 2,500 kote nchini.