Kenya yathibitisha visa 314 vya Mpox maambukizi yakiongezeka
Kenya imethibitisha jumla ya visa 314 vya ugonjwa wa Mpox kufikia Julai 31, 2025, ikiwa ni ongezeko kubwa la maambukizi mwaka mmoja tangu kisa cha kwanza kugunduliwa katika mpaka wa Taita-Taveta, Waziri wa Afya Dkt Aden Duale ametangaza.
Mlipuko huo ulianza Julai 31, 2024, pale mtu aliyekuwa akisafiri kutoka Uganda kuelekea Rwanda kupitia Kenya alipogunduliwa kuwa na Mpox katika kituo cha mpaka cha Taita-Taveta. Tangu hapo, ugonjwa huo umesambaa hadi kaunti 22 licha ya juhudi kabambe za kudhibiti maambukizi zinazoendeshwa na Wizara ya Afya.
Kaunti ya Mombasa inaongoza kwa kuwa na visa vingi zaidi vya Mpox, ikirekodi visa 146, ikifuatiwa na Busia (63), Nakuru (21), Kilifi (19), Nairobi (17), na Makueni (13). Taita-Taveta na Uasin Gishu zimeripoti visa vitano kila moja, huku Bungoma ikiwa na visa vinne. Kaunti za Kajiado, Kakamega na Kiambu kila moja imerekodi visa vitatu.
Kaunti za Kericho na Machakos zimeripoti visa viwili kila moja, ilhali Migori, Kisii, Kirinyaga, Isiolo, Kitui, Narok, Baringo na Trans-Nzoia zimeripoti kisa kimoja kila moja.
Wizara ya Afya ilieleza Ijumaa kuwa visa vinne vipya viliripotiwa ndani ya saa 24 zilizopita—viwili Mombasa na kimoja Nairobi.
“Kwa sasa, jumla ya wagonjwa 33 wamelazwa hospitalini huku 54 wakiwa kwenye uangalizi nyumbani. Zaidi ya hayo, wagonjwa 222 wamepona kabisa. Kwa masikitiko, wagonjwa watano wamepoteza maisha tangu kuzuka kwa ugonjwa huu, sawa na asilimia 1.6 ya waliopata maambukizi,” alisema Waziri Duale kwenye taarifa rasmi.
Juhudi za kufuatilia waliokaribiana na wagonjwa zimebaini watu 422 walitagusana na waliothibitishwa kuwa na Mpox. Kati yao, 392 wamekamilisha kipindi cha ufuatiliaji cha siku 21, huku waliobaki wakiendelea kufuatiliwa.
Dkt Duale amewasihi wananchi wazingatie maagizo ya afya ya umma na kutafuta taarifa kutoka kwa wataalamu wa afya waliohitimu. Taarifa rasmi zinaweza kupatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Afya au kupitia nambari za msaada: *719, 719#, 0729 471 414, na 0732 353 535.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA