• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Mfumo wa kidijitali wa maegesho JKIA wasimamishwa

Mfumo wa kidijitali wa maegesho JKIA wasimamishwa

Na BERNARDINE MUTANU

Bodi ya Kusimamia Tathmini ya Uagizaji kwa Umma (PPARB) imesimamisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (KAA) kusakini, kuendesha na kuweka mfumo wa dijitali katika maegesho ya magari ya kibinafsi katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Kulingana na PPARB, KAA ilikataa kufuata sheria za uagizaji katika kutoa tenda kutekeleza kazi hiyo kwa kampuni ya Kenya Airports Parking Services (KAPS), Septemba mwaka jana.

Kutokana na hilo bodi hiyo imefutilia mbali kandarasi hiyo. KAPS iliibuka mshindi miongoni mwa kampuni zingine sita zilizotuma maombi kuzingatiwa katika kandarasi hiyo.

Sasa KAA inahitajika kutathmini upya waombaji hao na kutoa kandarasi nyingine.

“Barua ya kutolewa kwa kandarasi hiyo iliyoandikwa Januari 3, 2019 kwa kampuni ya Kenya Airports Parking Services imefutilia mbali na kuwekwa kando,” alisema wakili wa bodi hiyo Faith Waigwa katika barua iliyoandikwa Januari 31, 2019.

“Hivyo KAA imeagizwa kutathmini upya kandarasi hiyo na kupata ada bora zaidi katika muda wa siku 14 kuanzia siku ya kufanya uamuzi huu,” alisema katika barua hiyo.

Kampuni zingine zilizotuma maombi ni Mason Services Limited ikishirikiana na Qntra Technology, Automatic Park Services Ltd, Atlancis Technologies, Paytech Ltd, Com Twenty One joint ikishirikiana na Servest Facilities Services Ltd, na Endeavour Africa Kenya Ltd ikishirikiana na East African Parking Ltd.

You can share this post!

KBL yaondolea kampuni pinzani visiki vya usambazaji wa pombe

Kaunti 10 zenye bidii ya kuiletea Kenya mapato

adminleo