Wito wazazi wawe macho na kuwalinda wanao wakati wa likizo
DIWANI wa wadi wa Nairobi South, Bi Waithera Chege ametoa wito kwa wazazi kuwa makini na malezi ya wanao wakiwa likizoni.
Akizungumza Jumanne, Agosti 12, 2025 wakati wa hafla ya kusambaza misaada mbalimbali kwa wakazi wa eneo hilo ili kuimarisha biashara zao chini ya mpango wa Empowerment Program, Bi Chege alisema kuwa baadhi ya wanafunzi hupotea njia hasa wakati wa likizo.
Bi Chege alisema wazazi wanapaswa kuzungumza na wanao mara kwa mara kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwahimiza kusoma kwa bidii ili kuimarisha maisha yao ya baadaye.
“Likizo hii ni fupi lakini inaweza kuharibu maisha ya mtoto iwapo mzazi hatakuwa makini. Zungumzeni nao kuhusu hatari za mihadarati na wawahimize kurejea shuleni wakiwa na malengo mapya ya kupata alama bora,” alisema Bi Chege.
Kando na hayo aliwahimiza wanafunzi kuwatii wazazi wao na kusoma kwa bidii.
Wakati wa hafla hiyo, Bi Chege aligawa wakazi vifaa kama vile mashine za kuosha magari na vifaa vya kuchomelea.
Mmoja wa walionufaika, Bw Peter Ouma, ambaye alipokea mashine ya kuosha magari, alisema msaada huo utabadilisha maisha yake.
“Sasa nina uhakika biashara yangu itakua kwa kasi. Nashukuru serikali na viongozi wetu kwa kutuletea mpango huu mashinani,” alisema Bw Ouma.
Wakazi walioshiriki hafla hiyo walitaja mpango huo kuwa wa manufaa makubwa kwa mwananchi wa kawaida kwani unawawezesha kupata kipato cha kujikimu na kuendeleza familia zao.