Jamvi La Siasa

Gachagua aiga mbinu ya Raila ya kutoweka na kurudi kwa mbwembwe

Na  JUSTUS WANGA, BENSON MATHEKA August 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HATA kabla ya ndege yake kutoka anga ya Amerika, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, amepanga kwa ustadi tamasha la kurudi nyumbani: umati wa wafuasi katika uwanja wa ndege, magari ya televisheni, na bendera nyingi za chama.

Ni mpango alioiga moja kwa moja kutoka historia ya siasa za Kenya, siasa za kutoweka na kurudi kwa heshima ambapo kiongozi hujificha kwa muda na kisha kurudi kwa mbwembwe.

Tangu zamani, wanasiasa wa Kenya wamekuwa wakitumia mbinu hii, ziara ndefu nje ya nchi, na kurudi kisha kurekebisha hali yao kisiasa.

Kenneth Matiba, Mwai Kibaki, Raila Odinga na Rais wa pili wa Jamhuri Daniel Moi wote wameitumia mbinu hii.

Bw Gachagua, alikatiza ziara yake ya miezi miwili nchini Amerika baada ya wiki nne tu, akitoa sababu kwamba ni lazima arudi nyumbani kuongoza chama chake kipya cha Democracy for Citizens’ (DCP) katika uchaguzi mdogo wa Novemba.

Bw Odinga amekuwa akitumia mbinu hii kikamilifu tangu miaka ya 1990, akitoweka pale siasa zilipokuwa zikichacha na kurudi kuongoza mikutano mikubwa.

Alifanya hivyo mwaka 2014, aliporudi baada ya kushindwa vibaya kwenye uchaguzi wa 2013 na Uhuru Kenyatta. Bw Odinga alikuwa waziri mkuu na Bw Kenyatta mmoja wa manaibu wake wawili katika serikali ya muungano chini ya Rais Kibaki.

Alikaa nje ya nchi kwa miezi miwili na kurudi kwake kulisherehekewa kwa hashtag maarufu mitandaoni, #BabaWhileYouWereAway. Ziara hiyo ilikuwa nafuu kwake na nafasi ya kupanga hatua inayofuata.

“Nanaleta salamu kutoka kwa Rais wa Amerika Barack Obama Jnr,” alisema Bw Odinga huku umati ukishangilia.

Kenneth Matiba alitumia kutoweka kwake baada ya kukamatwa bila kushtakiwa, akabadilisha mateso kuwa mtaji wa kisiasa.

Rais Moi alikuwa amemfunga kati ya Julai 1990 na Juni 1991. Baadaye aliondoka kwenda London na kurudi Mei 2, 1992 baada ya miezi kadhaa huko.

Na kutoweka kwa Mwai Kibaki kupata matibabu baada ya ajali ya barabarani kulikua muhimu kabla ya uchaguzi wa 2002. Alirudi na kupokelewa kwa mbwembwe na baadaye akashinda kwa wingi katika uchaguzi wa urais wa 2002.

Prof Macharia Munene, mwanahistoria ambaye amesoma mbinu za kisiasa za wanasiasa wa Kenya wanaosafiri nje na kupanga kurudi kwa heshima, anatoa hukumu kali.

“Kutoweka kunaunda hamu, hiyo haiwezi kupingwa,” alisema katika mahojiano.

“Lakini hamu si sawa na mamlaka,” asema.

Kwa Bw Gachagua, swali ni kwa nini anarudi sasa baada ya ahadi ya kurejea ndani ya miezi miwili?

Kurudi kwa Bw Gachagua kunaweza kuzima au kuzua mgawanyiko katika upinzani. Nguvu yake ni uwezo wa kuvutia umati hasa katika Mlima Kenya lakini doa yake ni matusi yanayogawa.

Prof Munene anayaonya kwamba siasa za kinywa-chungu hazivutii wapiga kura wasio na msimamo wa wazi.