Msisimko kwa Upinzani, tahadhari kwa Serikali Gachagua akirejea nchini leo
HALI ya msisimko inatarajiwa leo katika ulingo wa siasa nchini kufuatia kurudi kwa aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua kutoka Amerika ambako amekuwa ziarani kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Huku akitarajiwa kupokewa kwa mbwembwe na viongozi wa upinzani na wafuasi wake, maafisa wa usalama wamewekwa katika hali ya tahadhari.
Naibu kiongozi wa chama cha Gachagua cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Cleophas Malala, alisema msafara wa amani umepangwa kuanzia JKIA hadi kati kati mwa jiji la Nairobi, ambapo Bw Gachagua atahutubia wafuasi wake katika maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa Bw Malala, ndege itakayombeba Gachagua inatarajiwa kutua JKIA alasiri, na tayari wafuasi wake wamehimizwa kufika katika uwanja huo kuanzia saa mbili asubuhi kwa maandalizi ya mapokezi.
“Tunatarajia wafuasi wetu kujitokeza kwa wingi kuanzia asubuhi mapema. Tutakuwa na maandamano ya amani kumkaribisha kiongozi wetu kutoka JKIA hadi jiji kuu,” alisema Malala.
Hata hivyo, DCP imedai kuna njama ya kuvuruga maandamano hayo ya amani.
“Tuna habari kwamba, kuna watu wanaopanga kuvuruga maandamano haya. Tunatoa wito kwa idara za usalama kulinda amani na kuwakamata wahalifu wowote,” akaongeza.
Inatarajiwa kuwa Gachagua atahutubia umma, akihitimisha msafara wake katika uwanja wa Kamukunji au Uhuru Park, kulingana na mipango ya mwisho.
Viongozi wengine wa upinzani pia wamethibitisha kuhudhuria hafla hiyo ya kumkaribisha Gachagua.
Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, jana alisema kuwa Gachagua atashughulikiwa kama raia mwingine yeyote atakaporejea nchini.
“Ni ujio wa kawaida. Kazi yetu ni kuhakikisha usalama na sheria inazingatiwa. Yeyote atakayekiuka sheria atakamatwa,” alisema Bw Kanja.
Aliongeza kuwa Gachagua hayuko juu ya sheria, na endapo atahusishwa na uvunjaji wa sheria, atahitajika kurekodi taarifa pindi atakapotua nchini.
“Tunaongozwa na sheria. Iwapo kuna sheria aliyovunja, atachukuliwa hatua kama raia mwingine yeyote,” akaongeza.
Bw Kanja alikuwa ameandamana na Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Raymond Omollo na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI), Amin Mohammed, wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uongozi kwa makamanda wa polisi.
Tahadhari hii imejiri baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kuagiza maafisa wa usalama Jumanne kujiandaa kwa uwezekano wa vurugu, akimtaja Gachagua kama anayeweza kuchochea ghasia kupitia mikutano yake ya kisiasa.
“Ujio wake ni tishio la usalama. Naagiza vikosi vyetu kujiandaa kwa hali ya sintofahamu,” alisema Murkomen. Aliongeza kuwa maandamano ambayo yalikuwa yamepungua huenda yakarudi kwa nguvu kufuatia kurejea kwake.
Hata hivyo, Murkomen alikanusha madai kuwa serikali inapanga kumkamata Gachagua.
Akiwa nchini Amerika, Gachagua alitoa madai ya kutatanisha kuwa serikali ya Kenya ina uhusiano na makundi ya kigaidi pamoja na waasi kutoka Sudan — madai aliyosema atawasilisha kwa wachunguzi wa kimataifa.
“Sioni haja ya kushirikiana na vyombo vya uchunguzi vya Kenya. Nitatoa ushahidi wangu kwa mashirika ya Amerika pekee,” alisema.
Gachagua aliyeondolewa madarakani kupitia Bunge mnamo Oktoba mwaka jana, na kuwa Naibu Rais wa kwanza kuondolewa kupitia mchakato huo na wafuasi wake hasa kutoka eneo la Mlima Kenya walitafsiri hatua hiyo kama usaliti wa kisiasa.
Wandani wake sasa wanapanga kumkaribiasha kwa mbwembwe akirejea kwa kile kinachoonekana kama kupiga jeki upinzani katika kukosoa serikali.
Mbunge wa Tetu Geoffrey Wandeto alisema: “Huyu ndiye mgombea wetu wa urais 2027 kutoka Mlima Kenya. Tutakuwa na zaidi ya watu 20,000 kumpokea kutoka Uwanja wa Ndege wa JKIA hadi Kamukunji.”
Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia alionya wanaompuuzilia mbali Gachagua: “Aliangushwa kwa matumaini kuwa angefifia, lakini leo anathibitisha kuwa ana ushawishi.”
Kamishna wa Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa Wambui Nyutu alikosoa mashirika ya serikali kwa kumtishia Gachagua na kumtaka aende kuhojiwa.
Mbunge wa Kigumo Joseph Munyoro alitaja kurejea kwa Gachagua kama “kuzaliwa upya kwa matumaini” na mwanzo mpya wa harakati za kisiasa kuelekea 2027.
RIPOTI ZA NDUBI MOTURI, KEVIN CHERUIYOT, MWANGI MUIRURI