Obado aililia mahakama imhurumie
Na RICHARD MUNGUTI
GAVANA wa Migori Alhamisi aliomba mahakama kuu ibatilishe masharti aliyowekewa ya kutotembea nje ya kaunti hiyo alipoachiliwa kwa dhamana.
Jaji Jessie Lesiit alifahamishwa Gavana Obado ndiye mwenyekiti wa kamati ya magavana kuhusu kilimo na mara kwa mara anatakiwa kutembea mataifa ya ng’ambo kuhudhuria vikao.
Bw Obado anayeshtakiwa kwa kumuua mpenziwe Sharon Otieno na mwanawe ambaye alikuwa hajazaliwa aliomba akubaliwe kuchukua pasipoti kila anapotakiwa kusafiri kisha arudishe.
Mahakama ilielezwa kwamba Bw Obado akiwa mwenyekiti wa kamati ya kilimo ya baraza la magavana nchini anatakiwa kuhudhuria kongamano za kimataifa na pia maeneo ya Afrika mashariki.
Mahakama pia ilielezwa wakati Bw Obado anapo safari kutoka nyumbani hadi Nairobi inabidi atumie njia nyingine badala ya kutumia njia inayopitia Homabay na ambayo ni fupi.
“Naomba mahakama ibatilishe masharti ya dhamana inikubalie kupitia Homabay kwa vile ni njia fupi kufika Nairobi,” wakili Cliff Ombeta alimweleza Jaji Jessie Lesiit.
Bw Obado ameshtakiwa pamoja na aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na afisa mkuu kaunti ya Migori Bw Caspal Obiero.
Bw Obado aliachiliwa kwa dhamana ya Sh5milioni prds tasilimu na wadhamini wawili wa kiasi hicho.
Kiongozi wa mashtaka Bw Alexander Muteti alimweleza jaji tayari washtakiwa wamepewa nakala za mashahidi 10 na kwamba taarifa zilizosalia zenye kurasa 1000 zahitaji kukaguliwa na mtaalam aliyesafarini ng’ambo na anatarajiwa kurudi nchini wiki ijayo.
Kesi hiyo itatajwa Machi 20.