Jamvi La Siasa

Wabunge walia kuvuliwa nguo kwa dai wanapenda mlungula

Na JUSTUS OCHIENG August 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Bunge la Kenya limetikisiwa kisiasa na pia machoni mwa umma tangu Rais William Ruto alipozidisha mashambulishi yake kwa wabunge akiwahusisha na ufisadi, huku kiongozi wa ODM, Raila Odinga, akiibua tena wito wa kuwapokonya Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo bunge (NG‑CDF), na kupeleka fedha hizo moja kwa moja kwa kaunti.

Kumulikwa kwa bunge kumejiri wakati ambapo uhusiano kati ya Serikali Kuu na Bunge umekuwa tete. Alhamisi, Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetang’ula, aliwaambia wabunge wakati wa ufunguzi rasmi wa Kikao cha 3 cha uongozi wa Bunge la 13 huko Mombasa kwamba mijadala ya hivi karibuni imepaka tope hadhi ya Bunge kwa tuhuma za wabunge kupokea rushwa katika kutunga sheria.

“Ninachukulia madai haya kama uvumi, lakini kama taasisi hatuwezi kupuuza hisia zinazoongezeka kwamba ufisadi umeingia katika mchakato wa kutunga sheria,” alisema. Aliongeza:“Zaidi ya wakati mwingine wowote, kumekuwa na shaka kuhusu uadilifu wetu kama Bunge. Bila uadilifu, viongozi hupoteza uaminifu mbele ya watu wao. Bila uadilifu, hata kazi iliyofanywa kwa umakini haiwezi kuleta athari. Bila uadilifu, uongozi unafeli.”

Katika mikutano ya umma, Rais Ruto amewataja wabunge kama walinzi wa mitandao ya ufisadi, na kuwaambia kuwa shughuli za uchunguzi zimegeuzwa kuwa njia za kujinufaisha binafsi.

Alidai kwamba baadhi ya wabunge walinunuliwa kwa mamilioni ya shilingi ili kulemaza sheria muhimu kama ile ya kupambana na ulanguzi wa fedha.“Je, mnajua kuwa baadhi ya wanachama wa kamati yenu walipokea Sh10 milioni ili msipitishe ile sheria ya kuzuia ulanguzi wa pesa? Je, mlipokea pesa hizo?” aliuliza.

Kwa wakati huu ambapo Bunge linakumbwa na shinikizo kubwa kuhalalisha mabilioni inayojitengea kila mwaka huku huduma mashinani zikidorora, ukaguzi wa matumizi ya fedha unaoendeshwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali umebaini mianya mingi ya ufisadi kuanzia marupurupu ya kutatanisha, bajeti kubwa hadi matumizi yasiyoeleweka.

Hata hivyo, Naibu Spika Gladys Boss Shollei ametetea taasisi hiyo akisema Kamati za Bunge ndizo “injini ya shughuli za Bunge,” akibainisha kuwa ziliendesha vikao 2,115 – vikiwemo 820 vya Kamati za Ukaguzi, Bajeti na Kamati za Kawaida, na 1,295 vya Kamati za Kisekta.

“Katika jukumu la usimamizi pekee, Kamati zilichambua ripoti 648 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, na kuimarisha ufuatiliaji wa hoja za ukaguzi,” alisema katika kikao cha wabunge mjini Mombasa.

Lakini maswali yanazidi kuibuka. Kinara wa ODM Raila Odinga ameibua tena mjadala tata kuhusu NG-CDF. Mahakama ya Juu iliamua mwaka wa 2022 kuwa NG-CDF ni kinyume cha katiba kwa kuwaruhusu wabunge kusimamia fedha moja kwa moja.

Odinga anasisitiza kuwa fedha hizo hazifai kufutiliwa mbali, bali zielekezwe kwa serikali za kaunti ili kuimarisha ugatuzi. Akitilia shaka juhudi za sasa za wabunge kutaka kuingiza CDF kwenye katiba kupitia ushirikishaji wa umma, alisema mchakato huo ni bure bila kura ya maamuzi ya kitaifa.

“CDF ni takriban asilimia 2.5 ya bajeti ya kitaifa. Hizo ni hela nyingi. Zikiingizwa kwa kaunti, mgao wao utaongezeka kutoka asilimia 15 hadi 17.5. Hii ni hatua bora ya kuimarisha ugatuzi,” alisema.

Kauli yake hata hivyo, ilipuuzwa na wabunge wanaoegemea upande wa Rais Ruto. Wakiongozwa na Mbunge wa Mwala na Katibu wa Kitaifa wa UDA Vincent Kawaya, walimtaja Odinga kuwa mnafiki kwa kupinga msimamo aliounga mkono alipokuwa kinara mwenza wa Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa (Nadco). Nadco ilipendekeza kuhalalishwa kwa NG-CDF, NGAAF na Hazina ya Usimamizi ya Seneti kupitia katiba.

Katika kikao hicho cha Mombasa, Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah alilalamikia kile alichokitaja kuwa “upotoshaji mkubwa wa habari” kuhusu kazi ya Bunge. Alieleza kuwa Bunge lilifanya vikao 79, likashughulikia miswada 65, kuwasilisha hoja 157, kuuliza maswali 116 kwa mawaziri, kuomba taarifa 296, kuchunguza Idara za kisheria 53, kuwasilisha karatasi 2,302 na kujadili ripoti 148 za kamati.

“Licha ya mafanikio haya, kazi yetu mara nyingi hudhoofishwa na habari za kupotosha. Iwapo wananchi hawatahusishwa ipasavyo na kazi ya Bunge, juhudi zetu zitakuwa bure,” alionya.

Katika mwelekeo mwingine, Bw Odinga alishutumu Seneti kwa kugeuza jukumu lake la usimamizi kuwa ‘bughudha’ kwa magavana. “Seneti haifai kuwa kama kituo cha polisi kwa magavana. Usimamizi usiwe wa kuvuruga utendakazi wa kaunti,” alisema, akisisitiza kuwa mabunge ya kaunti na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu ndio waangalizi halali wa fedha mashinani.

Wabunge wengine wameishutumu Baraza la Magavana (CoG) kwa kile walichokitaja kuwa kampeni iliyoratibiwa ya kudhoofisha hadhi ya Bunge. Mbunge mmoja kutoka Kaskazini mwa Kenya alisema, “Mjadala huu wa sasa kuhusu ufisadi Bungeni ulianzishwa baada ya Mkutano wa Ugatuzi. Ni wazi kuwa ni mojawapo ya vita vinavyoendeshwa na magavana dhidi ya Bunge.”

Mgongano huu wa misimamo Rais Ruto akiwataja wabunge kama wafisadi na Raila akitaka wapokonywe mamlaka ya kifedha huku akitetea magavana umeweka Bunge kwenye mizani ya kisiasa. Wachambuzi wanasema wawili hao wanajaribu kuelekeza mjadala wa kitaifa kuelekea uchaguzi wa 2027.

Wakili Willis Otieno naye alisema, “Rais anafaa kuwa mtu wa mwisho kulaumu Bunge. Kama ana taarifa za kijasusi kuhusu ufisadi, anapaswa kuzifikisha kwa idara za sheria. Kukosa kufanya hivyo kunamfanya kuwa mshiriki.”