Mashabiki wakosa adabu kutupiana kinyesi mechi ya Copa Sudamericana ikitibuka Argentina
BUENOS AIRES, ARGENTINA
KIOJA cha kutupiana kinyesi kiliharibu mechi ya Klabu Bingwa bara Amerika Kusini (Copa Sudamericana) baada ya ghasia kati ya mashabiki kuvuruga mchuano huo wa raundi ya 16 kati ya wenyeji Independiente na Universidad de Chile, jijini Buenos Aires hapo Jumatano usiku.
Machafuko hayo, ambayo yamelaaniwa vikali na Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino, yalisababisha mashabiki 19 wa Chile kukimbizwa hospitalini, wawili wakidungwa visu huku mmoja akiwa katika hali mbaya baada ya kuanguka kutoka sitaha – orofa – ya juu katika uga huo wa Libertadores de America.

Inaripotiwa kuwa zaidi ya watu 300 walikamatwa ingawa klabu ya Chile ilithibitisha 97 pekee. Vurugu zilianza wakati wa mapumziko mashabiki wakirusha grenedi ya mshtuko, mawe, vyoo, sinki na viti vya wageni kuelekeza chini katika eneo la mashabiki wa nyumbani.
Hali ilizorota kipindi cha pili baada ya mashabiki wa nyumbani wa Independiente kuvamia sehemu ya wageni, kuwapiga na hata kuvua nguo baadhi ya mashabiki wageni wa Universidad.
Shutuma kote kote
Rais Gabriel Boric wa Chile amelaani tukio hilo akilitaja kuwa “lisilokubalika” kutokana na ghasia na maandalizi duni. Balozi wa Chile nchini Argentina alithibitisha majeruhi kadhaa wa visu, huku mkurugenzi wa Universidad de Chile, Daniel Schapira, akieleza hali hiyo kama “watu wasio na akili” na kulaumu waandalizi kwa kuweka mashabiki wa kigeni juu ya wenyeji.
Rais wa klabu ya Independiente, Nestor Grindetti, alitetea mikakati ya kiusalama iliyoidhinishwa na Shirikisho la Soka la Amerika ya Kusini (Conmebol), na kunyooshea kidole cha lawama mashabiki wa Universidad kwa “kuharibu vyoo na kurusha vifaa.”
Hata hivyo, mwenzake wa klabu ya Universidad, Michael Clark, alijibu kwa kusema tukio hilo ni “janga” na kusisitiza kwamba si wakati wa kulaumiana.

Mechi hiyo, ambayo ilikuwa sare ya 1-1 huku Universidad wakiongoza kwa jumla ya mabao 2-1, ilighairiwa rasmi na Conmebol kwa sababu ya ukosefu wa ithibati za kiusalama. Conmebol iliongeza kuwa italipeleka suala hilo kwenye kamati yake ya nidhamu.
Kiungo wa Chile, Felipe Loyola, anayechezea Independiente alisema: “Kiwango hiki cha ghasia hakiwezi kuvumiliwa. Michezo si vurugu.”
Adhabu kali
Mechi hiyo, ambayo ilikuwa sare ya 1-1 huku Universidad wakiongoza kwa jumla ya mabao 2-1, ilighairiwa rasmi na Conmebol kwa sababu ya ukosefu wa ithibati za kiusalama. Conmebol iliongeza kuwa italipeleka suala hilo kwenye kamati yake ya nidhamu.
Rais Boric ameahidi kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za haraka za matibabu na kwamba haki za waliokamatwa zitalindwa, huku soka ya Amerika Kusini ikikumbwa tena na usiku wa vurugu za kutisha uwanjani.
Duru zinasema kuwa klabu zote mbili zitachukuliwa hatua kali inayoweza kujumuisha uwanja huo kufungwa, timu kucheza mechi bila mashabiki, faini, timu kutupwa nje ya dimba hilo pamoja na kupigwa marufuku kushiriki mashindano ya kimataifa kwa muda fulani.