Sababu za Kenya Moja Alliance kutaka kushirikiana na Kalonzo, Gachagua
MUUNGANO wa Kenya Moja Alliance, unaojumuisha kundi la wabunge vijana, umetangaza nia ya kushirikiana na viongozi wa upinzani wenye mawazo sawa na yao, akiwemo Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka, ili kuunda upinzani thabiti wa kumpinga Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Wakizungumza katika ibada ya Jumapili katika kanisa la Jesus Teaching Ministries linaloongozwa na Mchungaji Peter Manyuru eneo la Embakasi Mashariki, viongozi hao walidokeza kuwa zaidi ya wabunge 70 tayari wameonyesha nia ya kujiunga na muungano huo.
Wabunge hao, wakiongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, walieleza kuwa wamejipanga vyema kuelekea uchaguzi mkuu ujao, wakisema kuwa hata Serikali Jumuishi haiwezi kuzuia azma yao
Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Anthony Kibagendi, alisema kuwa watazunguza na viongozi wengine wa upinzani kama Gavana George Natembeya, Kalonzo Musyoka, Rigathi Gachagua, na Dkt Fred Matiang’i ili kuunda muungano wa kitaifa wa kupinga utawala wa sasa.
“Tumeamua kushikana mikono kuokoa taifa letu kutoka mikononi mwa serikali ya Kenya Kwanza. Ili kuwashinda, lazima tuungane. Naomba tuwalete wote pamoja Kalonzo, Gachagua, Natembeya, Matiang’i tushirikiane kuwaokoa Wakenya,” alisema Bw Kibagendi.
Bw Kibagendi alimshutumu Rais Ruto kwa kuongeza ushuru na kufanya gharama ya maisha kuwa ya kutisha kwa wananchi wa kawaida.
Seneta Sifuna alisema kuwa wabunge wa Kenya Moja wamekuwa wakipata vitisho kutoka kwa serikali ya sasa, lakini wataendelea kuungana bila kuyumbishwa.
“Tuko tayari hata kutoa maisha yetu kwa ajili ya ajenda tunayoamini. Hatutakubali kunyamazishwa,” alisema Sifuna.
Aidha, Sifuna alidai kuwa matamshi ya hivi majuzi ya Rais Ruto kuhusu Bunge kuwa “ngome ya ufisadi ” yalilenga viongozi wanaopinga ajenda ya serikali jumuishi.
Mbunge Babu Owino, kwa upande wake, alimkosoa Rais kwa kushindwa kukabiliana na ufisadi ndani ya serikali yake:
“Mheshimiwa Rais, ukitaka kushughulikia ufisadi, anza na watu walioko karibu nawe. La sivyo, tutaamini ufisadi unaanzia kwako. Badala ya kuunda jopo la mashirika mengi, teua watu wa Mungu kupigana na ufisadi,” alisema.
Katika tukio lililoibua mshangao, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi alijikuta katika hali ya aibu baada ya mchungaji Manyuru kukataa mchango wake wa Sh100,000, akisema kanisa hilo limeacha kupokea fedha kutoka kwa wabunge ili kuepuka lawama za “kushawishiwa.”
“Najua wapo waliokuja hapa kwa mara ya kwanza tangu tulipotangaza hatutapokea pesa kutoka kwa wabunge. Hatutaki kusemwa kuwa tunahongwa. Lakini tuko tayari kuja katika michango yenu,” alisema Mchungaji Manyuru.
alimkosoa Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kwa kutotoa majibu kuhusu vifo vya Kware na waliouawa wakati wa maandamano ya kizazi cha Gen Z.
Viongozi wengine ni pamoja na Mbunge wa Kaiti Joshua Kimilu, Mbunge wa Bomachoge Borabu Obadiah Barongo, na Mbunge wa Kitutu Masaba Clive Gisairo, Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, pamoja na madiwani mbalimbali.