Habari Mseto

Wabunge waikataza KQ kusimamia JKIA

February 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wamepinga mpango unaopendekezwa wa kuwezesha Shirika la Ndege Nchini (Kenya Airways-KQ) kutwaa usimamizi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) wakisema utaleta madhara mengi.

Wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) walisema mpango huo utasababisha watu wengi kupoteza nafasi zao za ajira ikiwa KQ itatwaa usimamizi wa JKIA. Wakati huu uwanja huo uko chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) ambalo ni shirika la serikali.

KAA huchuma faidi ya takriban Sh13.5 kila mwaka.

Wabunge hao wakiongozwa na mwenyekiti wa PIC Abdulswamad Nassir pia walisema kuwa KQ ina wenye hisa wa kigeni na endapo itatwaa JKIA hatua hiyo itakuwa sawa na kuuza mali ya Wakenya kwa wageni.

“Uwanja wa Ndege wa JKIA ni sura ya Kenya na hatutaki kuamka siku moja na kusikia kuwa imetwaliwa na wageni kupitia KQ. Tunafahamu kwamba kampuni ambayo ina hisa nyingi katika KQ ni KLM ambayo ni shirika la kigeni,” Bw Nassir akasema kwenye kikao na wanahabari Alhamisi katika majengo ya bunge, Nairobi.

KLM ni shirika la ndege la Uholanzi lenye makao yake makuu karibu na uwanja wa Ndege wa Armsterdam. Linamiliki asilimia 45 ya hisa katika Shirika la KQ huku serikali ya Kenya ikimilika asilimia 25 pekee ya hisa. Hisa zilizosalia zinamilikiwa na watu binafsi.

“Kwa misingi hii, huu mpango ni mbaya na tunataka kujua ni kwa nini serikali inauunga mkono bila kufanya uchunguzi kuhusu athari zake kwa taifa la Kenya,” akasema Bw Nassir ambaye ni Mbunge wa Mvita.

Mpango huo wa KQ kutwaa usimamizi wa JKIA na KAA, uko katika hati iliyoidhinishwa na baraza la mawaziri mnamo Juni mwaka jana.

Chini ya mpango huo KQ itatunza na kustawisha uwanja wa JKIA na miundo misingi mingine katika eneo hilo.

Ikiwa mpango huo utafaulu, KQ itaungana na KAA kwa lengo la kuiamarisha biashara katika uwanja huo na kugeuza Nairobi kuwa kitovu cha uchukuzi wa angani katika ukanda huu wa Afrika.

Hatua hiyo pia itapelekea kupanuka kwa huduma za mashirika mengine ya ndege yanayotumia JKIA, huduma za kuhifadhi na uchukuzi wa mizigo na utunzi wa miundo mbinu katika uwanja huo mkubwa zaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Chama cha wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi wa angani (KAWU) pia kilionekana kupinga mpango huo na ukaitisha mgomo. Hata hivyo, Waziri wa Uchukuzi James Macharia na Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU) waliingilia kati mzozo huo na kufaulu kuwashawishi wafanyakazi hao kusitisha mgomo huo “ili kutoa nafasi kwa majadiliano zaidi kuhusu mpango huo”.

Katibu Mkuu wa KAWU Moss Ndiema alisema kuwa wanahofia kuwa mpango huo utapelekea baadhi yao kupoteza kazi au kupunguziwa mishahara.