Demu abubujikwa machozi kugundua mpenzi wake ni mhalifu anayesakwa na polisi
MTWAPA, KILIFI
KIPUSA mmoja alijuta baada ya kugundua kuwa mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa moyo wake wote ni mhalifu aliyekuwa akisakwa na polisi.
Mwanadada huyo alifichua kwamba, alikutana na jamaa huyo kwenye mitandao ya kijamii miezi sita iliyopita, na tangu hapo walijenga uhusiano uliompa matumaini ya ndoa.
“Hakuwa na dalili zozote za kuwa mhalifu. Alikuwa mpole, mchangamfu na alikuwa na pesa. Aliniambia anafanya biashara ya kuuza magari Mombasa,” alisema kwa masikitiko.
Hata hivyo, hali ilibadilika alipofahamu jamaa ana kesi nyingi za uhalifu si tu Mombasa bali pia katika korti nyingine nchini.
Alidai mwanaume huyo alikuwa mtu wa kujifanya mpole kiasi kwamba ni vigumu kushuku mienendo yake ya uhalifu.
“Sijui kama nitampenda mwanaume tena hivi karibuni,” alisema huku akifuta machozi.