Habari za Kitaifa

Raia wa kigeni wavuna mabilioni nchini Wakenya wakihamia ng’ambo kwa ajira

Na  PATRICK ALUSHULA August 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Wageni wanaoishi na kufanya kazi nchini Kenya walituma jumla ya Sh91.84 bilioni kwao nyumbani katika kipindi kilichokamilika Desemba 2024—kiasi ambacho ni cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa.

Hii ni ishara kuwa wengi wao wanaendelea kufaulu kifedha, huku Wakenya wakizidi kuondoka nchini kutafuta maisha bora ughaibuni.

Takwimu mpya zilizotolewa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) zinaonyesha ongezeko la asilimia 5.58 kutoka Sh86.99 bilioni mwaka uliotangulia. Huu ni mwaka wa tano mfululizo ambapo kiasi cha fedha kinachotumwa na wageni kutoka Kenya kwenda mataifa yao kimeendelea kuongezeka, japo kasi ya ukuaji ilipungua ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 24.3 mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa CBK, sehemu kubwa ya fedha hizo zilitumwa kwenda mataifa ya Afrika Mashariki kupitia njia za kidijitali pamoja na kampuni 21 za huduma za kutuma pesa zilizosajiliwa nchini.

“Njia za kidijitali ndizo maarufu zaidi kwa sababu zinapatikana kwa urahisi na kasi ya kufikisha pesa kwa wanaolengwa,” ilisema CBK kwenye ripoti yake ya hivi punde kuhusu usimamizi wa sekta ya benki.

Hali hii inaonyesha kuwa kuna idadi kubwa ya wageni wanaotegemea Kenya kujipatia kipato, huku maelfu ya Wakenya wakihama nchini kutafuta kazi nje. Kenya ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo huruhusu uhamaji wa watu na bidhaa, jambo linalochochea mafanikio ya kiuchumi katika ukanda huu.

Kwa upande mwingine, Wakenya wamekuwa wakihamia mataifa kama Uingereza, Amerika, Canada na Saudi Arabia kwa wingi wakitafuta ajira na marupurupu mazuri. Kufikia mwisho wa 2023, Wizara ya Masuala ya Kigeni ilikadiria kuwa Wakenya wapatao milioni nne walikuwa wakiishi ughaibuni.

Katika kipindi hicho hicho, kiasi cha fedha kilichoingizwa nchini kutoka kwa Wakenya wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi kiliongezeka hadi Sh440.18 bilioni, kutoka Sh362.91 bilioni mwaka uliotangulia. Hii inamaanisha kuwa kwa kila Sh1 inayotoka Kenya, Sh5 huingia nchini kupitia raia walioko ughaibuni.

Hata hivyo, CBK inakiri kuwa takwimu hizi huenda hazijajumuisha uhalisia wote wa uhamishaji fedha, hasa kwa vile ripoti ya 2022 kutoka shirika la Financial Sector Deepening (FSD) Kenya ilionyesha kuwa asilimia 70 ya pesa zinazotumwa kati ya Kenya na mataifa jirani kama Tanzania na Uganda hupitia njia zisizo rasmi.

FSD ilibainisha kuwa watu wengi katika ukanda huu hutumia simu zaidi ya moja na mtandao, jambo linalorahisisha kutuma na kupokea fedha bila kutumia njia rasmi.

“Baadhi ya watu huficha miamala yao kwa makusudi ili kuepuka ushuru au kufanikisha shughuli haramu,” ilisema ripoti ya FSD.